Ibara 64
Madaraka ya kutunga Sheria
Bunge la Jamhuri ya Muungano · Bunge
(1)Mamlaka yote ya kutunga sheria juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara, yatakuw mikononi mwa Bunge.
(2)Mamlaka yoyote ya kutunga sheria katika Tanzania Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo mambo ya Muungano yatakuwa mikononi mwa Baraza la Wawakilishi.
(3)Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi inahusu jambo lolote katika Tanzania Zanzibar ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge, sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka na pia endapo sheria yoyote iliyotungwa na Bunge inahusu jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya Baraza la Wawakilishi, sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka.
(4)Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge kuhusu jambo lo lote haitatumika Tanzania Zanzibar ila kwa mujibu wa masharti yafuatayo-
(a)sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na vile vile Tanzania Zanzibar au iwe inabadilisha, kurekebisha au kufuta sheria inayotuka Tanzania Zanzibar; au
(b)sheria hiyo iwe inabadilisha au kurekebisha au kufuta sheria iliyokuwa inatumika tangu zamani Tanzania Bara ambayo ilikuwa inatumika pia Tanzania Zanzibar kwa mujibu wa Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ya mwaka 1964 au kwa mujibu wa Sheria yoyote ambayo ilitamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na vile vile Tanzania Zanzibar; au
(c)Sheria hiyo iwe inahusu mambo ya Muungano, na kila inapotajwa Tanzania katika Sheria yoyote ifahamike kuwa sheria hiyo itatumika katika Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Ufafanuzi uliotolewa na masharti ya ibara hii.
(5)Bila ya kuathiri kutumika kwa Katiba ya Zanzibar kwa mujibu wa Katiba hii kuhusu mambo yote ya Tanzania Zanzibar yasiyo Mambo ya Muungano, Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba itakuwa batili.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.12 ib.12
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.