Wakili Msomi

Ibara 106

Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na madaraka ya kutunga Sheria za Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar · Baraza la Wawakilishi la Zanzibar

(1)Kutakuwa na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Baraza la Wawakilishi litakuwa na sehemu mbili; sehemu moja itakuwa ni ya wajumbe wa Baraza hilo waliochaguliwa na kuteuliwa kwa namna itakavyoelezwa na masharti ya Katiba ya Zanzibar, ya mwaka 1984, na ambao watajulikana kama wajumbe Wawakilishi; sehemu nyingine ya Baraza la Wawakilishi itakuwa ni Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa mahsarti ya Katiba hii na masharti ya Katiba ya Zanzibar, ya mwaka 1984.

(2)Iwapo kwa mujibu wa mahsarti ya Katiba hii, masharti ya Katiba ya Zanzibar, ya mwaka 1984, au masharti ya sheria yoyote iliyowekwa na inayotumika Zanzibar, jambo lolote lahitaji kuamuliwa au kutekelezwa na sehemu zote mbili za Baraza la Wawakilishi, basi jambo hilo halitahesabiwa kuwa limeamuliwa na limetekelezwa ipasavyo ila mpaka liwe limeamuliwa au limetekelezwa na Wajumbe wawakilishi na vile vile Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanizbar, kwa mujibu wa madaraka yao kuhusu jambo hilo.

(3)Madaraka yote ya kutunga sheria katika Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo Mambo ya Muungano yatakuwa mikononi mwa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1980 Na.1 ib.93

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.