Wakili Msomi

Ibara 98

Utaratibu wa kubadilisha Katiba hii na baadhi ya sheria

Bunge la Jamhuri ya Muungano · Utaratibu, Madaraka na Haki za Bunge

(1)Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii kwa kufuata Kanuni zifuatazo:-

(a)Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii (isipokuwa yale yanayohusika na aya ya (b) ya ibara hii ndogo) au masharti yoyote ya sheria yoyote iliyotajwa katika Orodha ya Kwanza kwenye Nyongeza ya Pili utaungwa mkono kwa kura za Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote;

(b)Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii au masharti yoyote ya Sheria yoyote yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Orodha ya Pili kwenye Nyongeza ya Pili iliyoko mwishoni wa Katiba hii, utapitishwa tu iwapo utaungwa mkono kwa kura za Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Zanzibar.

(2)Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara ndogo ya (1) kubadilisha masharti ya Katiba hii au masharti ya sheria maana yake ifahamike kuwa ni pamoja na kurekebisha au kusahihisha masharti haya au kufuta na kuweka masharti mengine badala yake au kusisitiza au kubadilisha matumizi ya masharti hayo.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.14

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.