Ibara 97
Namna ya kutumia madaraka ya kutunga sheria
Bunge la Jamhuri ya Muungano · Utaratibu, Madaraka na Haki za Bunge
(1)Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii, Bunge litatumia madaraka yake ya kutunga sheria kwa kufuata utaratibu wa kujadili na kupitisha Miswada ya Sheria ambayo hatimaye itabidi ipate kibali cha Rais, na Muswada hautakuwa Sheria mpaka uwe umepitishwa na Bunge na kukubaliwa na Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara hii.
(2)Baada ya Muswada kuwasilishwa kwa Rais kwa ajili ya kupata kibali chake, Rais aweza kuukubali au kukataa kuukubali, na iwapo Rais atakataa kuukubali Muswada basi ataurudisha kwa Bunge pamoja na maelezo ya sababu zake za kukataa kuukubali Muswada huo.
(3)Baada ya Muswada kurudishwa kwa Bunge kwa mujibu wa masharti ya ibara hii, hauwezi kupelekwa tena kwa Rais kwa ajili ya kupata kibali chake kabla kumalizika muda wa miezi sita tangu uliporudishwa, isipokuwa kama katika hatua yake ya mwisho kwenye Bunge kabla haujapelekwa tena kwa Rais Muswada huo umeungwa mkono na Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote.
(4)Iwapo Muswada umerudishwa kwa Bunge na Rais, halafu ukaungwa mkono kwenye Bunge na Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote kama ilivyoelezwa katika ibara ndogo ya (3) na kupelekwa kwa Rais kwa ajili ya kupata kibali chake kwa mara ya pili kabla haujamalizika muda wa miezi sita tangu uliporudishwa, basi Rais atatakiwa kuukubali Muswada huo kabla ya kumalizika muda wa siku ishirini na moja tangu Muswada huo ulipowasilishwa kwake la sivyo basi itabidi alivunje Bunge.
(5)Masharti yaliyomo katika ibara hii au katika ibara ya 64 ya Katiba hii hayatalizuia Bunge kutunga sheria na kuweka masharti ambayo yaweza kukabidhi kwa mtu yeyote au kwa idara yoyote ya Serikali madaraka ya kuweka Kanuni za nguvu ya kisheria au kuzipa nguvu ya kisheria Kanuni zozote zilizowekwa na mtu yeyote au idara yoyote ya Serikali.
Marejeo ya marekebisho: sheria ya 1984 Na.15 ib.4
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.