Wakili Msomi

Ibara 63

Madaraka ya Bunge

Bunge la Jamhuri ya Muungano · Bunge

(1)Rais kama sehemu moja ya Bunge atatekeleza madaraka yote aliyokabidhiwa na Katiba hii kwa ajili hiyo.

(2)Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.

(3)Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza-

(a)kumuuliza Waziri yeyoyote swali lo lote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake;

(b)kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti;

(c)kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo;

(d)kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kuwapo sheria;

(e)kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.12 Sheria ya 1992 Na.4 ib.17 Sheria ya 1992 Na.20 ib.11

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.