Wakili Msomi

Ibara 34

Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mamlaka yake

Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Rais

(1)Kutakuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano, na pia juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara.

(2)Mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano yatahusu utekelezaji na hifadhi ya Katiba hii na pia mambo mengineyo yote ambayo Bunge lina mamlaka ya kuyatungia sheria.

(3)Mamlaka yote ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano, na pia juu ya mambo mengineyo yote yahusuyo Tanzania Bara, yatakuwa mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

(4)Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, madaraka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano yatatekelezwa ama na Rais mwenyewe moja kwa moja au kwa kukasimu madaraka hayo kwa watu wengine wenye madaraka katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

(5)Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika ibara hii hayatahesabiwa kwamba-

(a)yanahamishia kwa Rais madaraka yoyote ya kisheria yaliyowekwa na sheria mikononi mwa mtu au mamlaka yoyote ambayo si Rais; au

(b)yanalizuia Bunge kukabidhi madaraka yoyote ya kisheria mikononi mwa mtu au watu au mamlaka yoyote ambayo si Rais.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.9

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.