Wakili Msomi

Ibara 4

Utekelezaji wa shughuli za Mamlaka ya Nchi

Jamhuri ya Muungano, Vyama vya Siasa, Watu na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea · Jamhuri ya Muungano na Watu

(1)Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji, vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki, na pia vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma.

(2)Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vitakuwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, vyombo vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki vitakuwa ni Idara ya Mahakama ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Idara ya Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge na Baraza la Wawakilishi.

(3)Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Jamhuri ya Muungano, na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo vilivyotajwa katika ibara hii, kutakuwa na Mambo ya Muungano kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza iliyoko mwishoni mwa Katiba hii, na pia kutakuwa na Mambo yasiyo ya Muungano ambayo ni mambo mengine yote yasiyo Mambo ya Muungano.

(4)Kila chombo kilichotajwa katika ibara hii kitaundwa na kutekeleza majukumu yake kwa kufuata masharti mengine yaliyomo katika Katiba hii.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.6

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.