Wakili Msomi

Ibara 5

Haki ya kupiga kura

Jamhuri ya Muungano, Vyama vya Siasa, Watu na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea · Jamhuri ya Muungano na Watu

(1)Kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofaywa Tanzania na wananchi. Na haki hii itatumiwa kwa kufuata masharti ya ibara ndogo ya (2) pamoja na masharti mengineyo ya Katiba hii na ya Sheria inayotumika nchini Tanzania kuhusu mambo ya uchaguzi.

(2)Bunge laweza kutunga sheria na kuweka masharti yanayoweza kuzuia raia asitumie haki ya kupiga kura kutokana na yoyote kati ya sababu zifuatazo, yaani raia huyo-

(a)kuwa na uraia wa nchi nyingine;

(b)kuwa na ugonjwa wa akili;

(c)kutiwa hatiani kwa makosa fulani ya jinai;

(d)kukosa au kushindwa kuthibitisha au kutoa kitambulisho cha umri, uraia au uandikishwaji kama mpiga kura,

mbali na sababu hizo hakuna sababu nyingine yoyote inayoweza kumzuia raia asitumie haki ya kupiga kura.

(3)Bunge litatunga Sheria ya Uchaguzi na kuweka masharti kuhusu mambo yafuatayo-

(a)kuanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga kura na kuweka utaratibu wa kurekebisha yaliyomo katika Daftari hilo;

(b)kutaja sehemu na nyakati za kuandikisha wapiga kura na kupiga kura;

(c)utaratibu wa kumwezesha mpiga kura aliyejiandikisha sehemu moja kupiga kura sehemu nyingine na kutaja masharti ya utekelezaji wa utaratibu huo;

(d)kutaja kazi na shughuli za Tume ya Uchaguzi na utaratibu wa kila uchaguzi ambao utaendeshwa chini ya uongozi na usimamizi wa Tume ya Uchaguzi.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.6 Sheria ya 2000 Na.3 ib.4

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.