Wakili Msomi

Ibara 67

Sifa za mtu kuwa Mbunge

Bunge la Jamhuri ya Muungano · Wabunge, Wilaya ya Uchaguzi na Uchaguzi wa Wabunge

(1)Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo-

(a)ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja, na ambaye anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza;

(b)ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa;

(c)katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi hakuwahi kutiwa hatiani katika mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali.

(2)Mtu hatakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge-

(a)ikiwa mtu huyo anao au kwa hiari yake amejipatia uraia wa nchi nyingine yote; au

(b)ikiwa kwa mujibu wa sheria inayotumika katika Jamhuri ya Muungano imethibitishwa rasmi kwamba mtu huyo ana ugonjwa wa akili; au

(c)ikiwa mtu huyo amehukumiwa na Mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani kwa muda unaozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa, linaloambatana na utovu wa uaminifu; au

(d)ikiwa katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu amepata kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;

(e)bila ya kuingilia haki na uhuru wa mtu kuwa na maoni yake, kuamini dini atakayo, kushirikiana na wengine na kushiriki shughuli za umma kwa mujibu wa sheria za nchi, ikiwa mtu huyo si mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa;

(f)ikiwa mtu huyo ana masilahi yoyote katika mkataba wa Serikali wa aina yoyote aliyowekewa miiko maalum kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, na iwapo amekiuka miiko hiyo;

(g)ikiwa mtu huyo ameshika madaraka ya afisa mwandamizi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, isipokuwa madaraka ambayo Rais aweza au anatakiwa kukabidhi kwa Mbunge kwa mujibu wa Katiba hii au sheria iliyotungwa na Bunge;

(h)ikiwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge inayoshughulikia makosa yanayohusika na uchaguzi wa aina yoyote mtu huyo amezuiliwa kujiandikisha kama mpiga kura au kupiga kura katika uchaguzi wa Wabunge.

(3)Mtu hataweza kugombea uchaguzi kuwa Mbunge wa kuwakilisha jimbo la uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu wowote ikiwa wakati huo yeye amesimama katika uchaguzi kugombea kiti cha Rais, wala hataweza kugombea uchaguzi kuwa Mbunge katika uchaguzi mdogo wowote ikiwa yeye ni Rais.

(4)Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kuweka masharti yatakayomzuia mtu asichaguliwe kuwa Mbuge wa kuwakilisha jimbo la uchaguzi ikiwa mtu huyo ni mwenye madaraka yanayohusika na shughuli za kuongoza au kusimamia uchaguzi wa Wabunge au shughuli za uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Wabungel isipokuwa kwamba Sheria kama hiyo haiwezi kuweka masharti yatakayomzuia Spika wa Bunge asichaguliwe kuwa Mbunge wa kuwakilisha wilaya ya uchaguzi, wala masharti yatakayosababisha mtu aliyechaguliwa kuwa Spika kupoteza kiti hicho cha Spika au kiti chake cha kawaida katika Bunge.

(5)Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kuweka masharti yatakayomuzia mtu asichaguliwe kuwa Mbunge wa kuwakilisha wilaya ya uchaguzi kwa muda wowote utakaotajwa na Bunge (ili mradi muda huo usizidi miaka mitano) ikiwa mtu huyo atapatikana na hatia mbele ya mahakama kwa ajili ya aina yoyote ya makosa yatakayotajwa katika Sheria hiyo yanayohusika na uchaguzi wa Wabunge.

(6)Kwa madhumuni ya kutoa fursa ya kukata rufaa kwa mujibu wa Sheria kwa mtu yeyote aliyethibitishwa rasmi kisheria kuwa ana ugonjwa wa akili au aliyehukumiwa na kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani au aliyepatikana na hatia ya kosa lolote lililotajwa katika Sheria kwa mujibu wa ibara ndogo ya (5) ya ibara hii, Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kuweka masharti yatakayoeleza kwamba hiyo hukumu inayopingwa na mtu huyo haitakuwa na nguvu kwa ajili ya utekelezaji wa masharti ya ibara ndogo ya (2) au ya (5) ya ibara hii mpaka upite kwanza muda utakaotajwa katika sheria hiyo.

(7)Kanuni zifuatazo zitatumika kwa ajili ya ufafanuzi wa aya ya ( c), ya (d) na ya (e) za ibara ndogo ya (2) ya ibara hii, yaani-

(a)ikiwa mtu amepewa adhabu mbili au zaidi za kufungwa gerezani na imeamuliwa afungwe kwa muda wa mfululizo, basi adhabu hizo zitahesabiwa kama ni adhabu mbalimbali iwapo muda uliotajwa katika kila moja ya adhabu hizo hauzidi miezi sita; lakini iwapo muda uliotajwa katika adhabu yoyote kati ya adhabu hizo unazidi miezi sita basi adhabu hizo zote zitahesabiwa kama ni adhabu moja;

(b)ikiwa mtu atapewa adhabu ya kufungwa gerezani ikifahamika kuwa adhabu hiyo ya kifungo imetolewa badala ya adhabu ya kutozwa faini au imetolewa kwa sababu mtu huyo ameshindwa kulipa faini aliyoamriwa kulipa, basi muda wa kifungo cha namna hiyo hautahesabiwa.

(8)Katika aya ya (f) ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hii "mkataba wa Serikali" maana yake ni mapatano yoyote ya mkataba ambayo mmojawapo wa walioshiriki ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi Zanzibar au Idara yoyote ya Serikali hiyo au mtumishi yeyote wa Serikali aliyeshiriki kwa niaba ya Serikali.

[ibara ndogo ya (9), (10), (11) na ya 12 zimefutwa na Sheria Na.4 ya 1992 Ib.19 (d)]

(13)Kwa ajili ya ufafanuzi wa maelezo kuhusu sifa za uchaguzi yaliyomo katika ibara zifuatazo, kila itakapotajwa katika Katiba hii kwamba utekelezaji wa jambo lolote wahitaji mtu mwenye sifa za uchaguzi au mtu ambaye hakupoteza sifa za uchaguzi, basi, isipokuwa kama maelezo yahitajia vinginevyo, ifahamike kuwa sifa zinazohusika ni zile zinazomwezesha mtu kuchaguliwa kuwa Mbunge wa kuwakilisha jimbo la uchaguzi kama ilivyoelezwa katika ibara ndogo ya (a) ya ibara hii.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.13 Sheria ya 1992 Na.4 ib.19 Sheria ya 1994 Na.34 ib.13 Sheria ya 1995 Na.12 ib.10 Sheria ya 2000 Na.3 ib.12

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.