Ibara 83
Uamuzi wa suala kama mtu ni Mbunge au sivyo
Bunge la Jamhuri ya Muungano · Wabunge, Wilaya ya Uchaguzi na Uchaguzi wa Wabunge
(1)Kila shauri kwa ajili ya kupata uamuzi juu ya suala -
(a)kama uchaguzi au uteuzi wa mtu yeyote kuwa mbunge ulikuwa halali au sivyo; au
(b)kama Mbunge amekoma kuwa Mbunge na kiti chake katika Bunge ki wazi au hapana, litafunguliwa na kusikilizwa kwanza katika Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hii.
(2)Iwapo Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya ibra ya 41(3) ya Katiba hii imemtangaza Mbunge yeyote kwamba amechaguliwa kuwa Rais basi hakuna mahakama wala chombo chochote kingine kitakachochunguza zaidi suala lolote linalohusu kiti cha Mbunge huyo kuwa wazi.
(3)Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti kuhusu mambo yafuatayo -
(a)watu wanaoweza kufungua shauri katika Mahakama Kuu kwa ajili ya kupata uamuzi juu ya suala lolote kwa mujibu wa masharti ya ibara hii;
(b)sababu na nyakati za kufungua shauri la namna hiyo, utaratibu wa kufungua shauri na masharti yanayotakiwa yatimizwe kwa kila shauri kama hilo; na
(c)kutaja mamlaka ya Mahakama Kuu juu ya shauri kama hilo na kueleza utaratibu wa kuskiliza shauri lenyewe.
(4)Kutakuwa na haki ya kukata rufaa mbele ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu juu ya shauri lolote lililosikilizwa kwa mujibu wa mahsarti ya ibara hii.
Marejeo ya marekebisho: Sheria za 1979, Na.14 Ibara 8 1984 Na.15 Ibara 13 1990 Na.14 1992 Na.4 Ibara 30
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.