Ibara 78
Utaratibu wa Uchaguzi wa Wabunge Wanawake wa kuchaguliwa na Bunge
Bunge la Jamhuri ya Muungano · Wabunge, Wilaya ya Uchaguzi na Uchaguzi wa Wabunge
(1)Kwa madhumuni ya uchaguzi wa Wabunge, Wanawake waliotajwa katika ibara ya 66(1) (b), vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi, kwa kufuata utaratibu uliowekwa, vitapendekeza kwa Tume ya Uchaguzi majina ya wanawake kwa kuzingatia masharti ya uwiano wa uwakilishi baina ya vyama vilivyoshinda uchaguzi katika majimbo na kupata viti Bungeni. Tume ya Uchaguzi ikiridhika kuwa mtu yeyote aliyependekezwa anazo sifa za kuwa Mbunge itamtangaza kuwa amechaguliwa kuwa Mbunge, na masharti ya ibara ya 83 ya Katiba hii yatatumika kuhusu kuchaguliwa kwa mtu huyo kuwa Mbunge.
(2)Mtu yeyote hataweza kupendekezwa na chama chochote cha siasa kwa ajili ya uchaguzi kwa mujibu wa ibara hii ila tu iwapo anazo sifa za kustahili kuchaguliwa zilizotajwa na masharti ya ibara ya 67 ya Katiba hii.
(3)Majina ya watu waliopendekezwa kwa mujibu wa ibara ndogo ya (1) na Tume ya Uchaguzi yatatangazwa kama matokeo ya uchaguzi baada ya Tume ya Uchaguzi kuridhika kwamba masharti ya Katiba na Sheria yanayohusika yamezingatiwa.
(4)Orodha ya majina ya wagombea wanawake iliyowasilishwa kwa Tume ya Uchaguzi na kila chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu ndiyo itakayotumiwa na Tume ya Uchaguzi baada ya kushauriana na chama kinachohusika, kwa madhumuni ya kujaza nafasi yoyote ya Mbunge wa aina hii inapotokea wakati wowote katika maisha ya Bunge.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1992 Na.4 ib.26 Sheria ya 2000 Na.3 ib.16
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.