Ibara 77
Utaratibu wa Uchaguzi wa Wabunge wa Majimbo ya Uchaguzi
Bunge la Jamhuri ya Muungano · Wabunge, Wilaya ya Uchaguzi na Uchaguzi wa Wabunge
(1)Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi watachaguliwa na wananchi kwa kufuata masharti ya Katiba hii na vile vile masharti ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba hii inayoweka masharti kuhusu uchaguzi wa Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi.
(2)Isipokuwa pale ambapo Tume ya Uchaguzi, kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au Sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo, itaagiza vinginevyo, kutachaguliwa Mbunge mmoja tu katika jimbo la uchaguzi.
(3)Wagombea uchaguzi katika jimbo la uchaguzi watatakiwa watimize masharti yafuatayo-
(a)wawe wamependekezwa mmoja mmoja, na chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi katika jimbo hilo;
(b)wamewasilisha majina yao kwa Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Bunge au uliofafanuliwa na Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1992 Na.4 ib. 25
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.