Ibara 75
Majimbo ya Uchaguzi
Bunge la Jamhuri ya Muungano · Wabunge, Wilaya ya Uchaguzi na Uchaguzi wa Wabunge
(1)Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyo katika ibara hii, Jamhuri ya Muungano itagawanywa katika majimbo ya uchaguzi kwa idadi na kwa namna itakavyoamuliwa na Tume ya Uchaguzi baada ya kupata kibali cha Rais.
(2)Bila ya kuathiri sheria yoyote inayotumika kuhusu mambo hayo, Tume ya Uchaguzi, baada ya kupata kibali cha Rais itakuwa na mamlaka ya kuweka mipaka ya majimbo ya uchaguzi.
(3)Katika kuweka mipaka ya majimbo ya uchaguzi, Tume ya Uchaguzi itazingatia ipasavyo upatikanaji wa njia za mawasiliano, na pia hali ya kijiografia ya eneo linalokusudiwa kugawanywa katika majimbo ya uchaguzi.
(4)Bila ya kuathiri masharti ya Katiba hii na ya sheria yoyote inayohusika na mgawanyo wa nchi katika majimbo ya uchaguzi, Tume ya Uchaguzi yaweza mara kwa mara, na angalao kila baada ya miaka kumi, kuchunguza mgawanyo wa Jamhuri ya Muungano katika majimbo ya uchaguzi, na yaweza kubadilisha majimbo ya uchaguzi kama matokeo ya uchunguzi huo au kutokana na matokeo ya hesabu ya watu wote katika Jamhuri ya Muungano.
(5)Endapo baada ya uchunguzi kufanywa kuhusu mgawanyo wa Jamhuri ya Muungano katika majimbo ya uchaguzi kunafanyika mabadiliko katika majimbo ya uchaguzi, au katika idadi ya Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi au mabadiliko kwa idadi ya majimbo ya uchaguzi au idadi ya Wabunge, basi mabadiliko yatakayotokea katika idadi ya Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi yataanza kutumika wakati Bunge litakapovunjwa tena baada ya kutokea mabadiliko hayo ya idadi ya majimbo au idadi ya Wabunge katika majimbo ya uchaguzi.
(6)Bila kujali masharti mengineyo ya ibara hii, hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume katika utekelezaji wake wa kugawa Jamhuri ya Muungano katika majimbo ya uchaguzi.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1992 Na.4 ib.24
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.