Ibara 41
Utaratibu wa uchaguzi wa Rais
Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Rais
(1)Baada ya Bunge kuvunjwa au kukitokea jambo jingine lolote lililotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara ya 38 na inalazimu uchaguzi wa Rais kufanyika, kila chama cha siasa kinachopenda kushiriki katika uchaguzi wa Rais kitawasilisha kwa Tume ya Uchaguzi, kwa mujibu wa sheria, jina la mwanachama wake mmoja kinayetaka asimame kama mgombea katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na jina la mwananchama wake mwingine kinayempendekeza kwa nafasi ya Makamu wa Rais.
(2)Mapendekezo ya majina ya wagombea katika uchaguzi wa Rais yatawasilishwa kwa Tume ya Uchaguzi katika siku na saa itakayotajwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, na mtu hatakuwa amependekezwa kwa halali isipokuwa tu kama kupendekezwa kwake kunaungwa mkono na wananchi wapiga kura kwa idadi na kwa namna itakayotajwa na sheria iliyotungwa na Bunge.
(3)Endapo inapofika saa na siku iliyotajwa kwa ajili ya kuwasilisha mapendekezo ya majina ya wagombea, ni mgombea mmoja tu ambaye anapendekezwa kwa halali, Tume itawasilisha jina lake kwa wananchi, nao watapiga kura ya kumkubali au kumkataa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii na ya sheria iliyotungwa na Bunge.
(4)Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano utafanywa siku itakayoteuliwa na Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge.
(5)Mambo mengine yote yahusuyo utaratibu wa uchaguzi wa Rais yatakuwa kama itakavyofafanuliwa katika sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo.
(6)Mgombea yeyote wa kiti cha Rais atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa Rais iwapo tu amepata kura nyingi zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote.
(7)Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.
Marejeo ya marekebisho: Sheria Na.20 ya 1992 Na.20 ib.5 Sheria Na.34 ya 1994 Na.34 ib.10
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.