Wakili Msomi

Ibara 38

Uchaguzi wa Rais

Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Rais

(1)Rais atachaguliwa na wananchi kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na kwa mujibu wa sheria itakayoweka masharti kuhusu uchaguzi wa Rais ambayo itatungwa na Bunge kwa kufuata masharti ya Katiba hii.

(2)Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, kiti cha Rais kitakuwa ki wazi, na uchaguzi wa Rais utafanyika au nafasi hiyo itajazwa vinginevyo kwa mujibu wa Katiba hii, kadri itakavyokuwa, kila mara litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo:-

(a)baada ya Bunge kuvunjwa;

(b)baada ya Rais kujiuzulu bila ya kulivunja Bunge kwanza:

(c)baada ya Rais kupoteza sifa za kushika nafasi madaraka ya kuchaguliwa;

(d)baada ya Rais kushtakiwa Bungeni kwa mujibu wa Katiba hii, na kuondolewa katika madaraka;

(e)baada ya kuthibitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 37 ya Katiba hii kwamba Rais hawezi kumudu kazi na shughuli zake;

(f)baada ya Rais kufariki.

(3)Kiti cha Rais hakitahesabiwa kuwa kiwazi kwa sababu tu ya Bunge kupitisha hoja ya kutokuwa na imani kwa Waziri Mkuu.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.9 Sheria ya 1992 Na.20 ib.5 Sheria ya 1994 Na.34 ib.

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.