Wakili Msomi

Ibara 37

Utekelezaji wa kazi na shughuli za Rais n.k

Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Rais

(1)Mbali na kuzingatia masharti yaliyomo katika Katiba hii, na sheria za Jamhuri ya Muungano katika utendaji wa kazi na shughuli zake, Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote, isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au na sheria nyingine yoyote kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na mtu au mamlaka yoyote.

(2)Endapo Baraza la Mawaziri litaona kuwa Rais hawezi kumudu kazi zake kwa sababu ya maradhi ya mwili au ya akili, laweza kuwasilisha kwa Jaji Mkuu azimio la kumwomba Jaji Mkuu athibitishe kwamba Rais, kwa sababu ya maradhi ya mwili au ya akili hawezi kumudu kazi zake. Baada ya kupokea azimio kama hilo, Jaji Mkuu atateua bodi ya utabibu ya watu wasiopungua watatu atakaowateua kutoka miongoni mwa mabingwa wanaotambuliwa na sheria ya matababu ya Tanzania, na bodi hiyo itachunguza suala hilo na kumshauri Jaji Mkuu ipasavyo, naye aweza, baada ya kutafakari ushahidi wa kitabibu kuwasilisha kwa Spika hati ya kuthibitisha kwamba Rais kutokana na maradhi ya mwili au ya akili, hamudu kazi zake; na iwapo Jaji Mkuu hatabatilisha tamko hilo ndani ya siku saba kutokana na Rais kupata nafuu na kurejea kazini, basi itahesabiwa kwamba kiti cha Rais ki wazi, na masharti yaliyomo katika ibara ndogo ya (3) yatatumika.

(3)Ikitokea kwamba Kiti cha Rais ki wazi kutokana na masharti yaliyomo katika ibara ndogo ya (2) au endapo kiti cha Rais kiwazi kutokana na sababu nyingine yoyote, na endapo Rais atakuwa hayupo katika Jamhuri ya Muungano, kazi na shuhguli za Rais zitatekelezwa na mmoja wapo na wafuatao, kwa kufuata orodha kama ilivyopangwa, yaani-

(a)Makamu wa Rais au kama nafasi yake iwazi au kama naye hayupo au ni mgonjwa; basi.

(b)Spika wa Bunge au, kama nafasi yake iwazi au kama naye hayupo au ni mgonjwa; basi

(c)Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano.

(4)Endapo yeyote kati ya watu waliotajwa katika aya ya (b) na (c) za ibara ndogo ya (3) atatekeleza kazi na shughuli za Rais kutokana na sababu kwamba mtu mwingine anayemtangulia katika orodha hiyo hayupo, basi mtu huyo ataacha kutekeleza kazi na shughuli hizo mara tu mtu huyo mwingine anayemtangulia atakaporejea na akashika na kuanza kuteleza kazi na shughuli za Rais.

(5)Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano na kwa masharti yaliyoelezwa katika ibara ya 40, kisha baada ya kushauriana na chama cha siasa anachotoka Rais atapendekeza jina la mtu atakae kuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia hamsini ya Wabunge wote.

(6)Ifahamike kwamba kiti cha Rais hakitakuwa kiwazi na Rais hatahesabiwa kwamba hayuko katika Jamhuri ya Muungano endapo-

(a)atakuwa hayupo katika mji ambao ndio makao makuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano;

(b)atakuwa hayupo katika Jamhuri ya Muungano kwa kipindi cha muda wa saa ishirini na nne; au

(c)atakuwa ni mgonjwa lakini anatumaini kuwa atapata nafuu baada ya muda si mrefu.

(7)Iwapo kutatokea lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika ibara ndogo ya (6) na Rais akiona kuwa inafaa kuwakilisha madaraka yake kwa muda wa jambo hilo, basi aweza kutoa maagizo kwa maandishi ya kumteua yeyote kati ya watu waliotajwa katika aya ya (a) au ya (b) za ibara ndogo ya (3) ya ibara hii kwa ajili ya kutekeleza madaraka ya Rais wakati yeye hayupo au ni mgonjwa, na mtu huyo atakayeteuliwa atatekeleza madaraka hayo ya Rais kwa kufuata masharti yoyote yatakayowekwa na Rais; isipokuwa kwamba masharti yaliyomo katika ibara hii ndogo yafahamike kuwa hayapunguzi wala kuathiri uwezo wa Rais alionao kwa mujibu wa sheria nyingine yoyote wa kuwakilisha madaraka yake kwa mtu mwingine yeyote.

(8)Rais aweza, akiona inafaa kufanya hivyo, kumwagiza kwa maandishi Waziri yeyote kutekeleza kazi na shughuli zozote za Rais ambazo Rais atazitaja katika maagizo yake na Waziri aliyeagizwa hivyo kwa mujibu wa masharti ya ibara hii ndogo, atakuwa na mamlaka ya kutekeleza kazi na shughuli hizo kwa kufuata masharti yoyote yaliyowekwa na Rais, lakini bila ya kujali masharti ya sheria nyingine yoyote; isipokuwa kwamba-

(a)Rais hatakuwa na mamlaka ya kuwakilisha kwa Waziri kwa mujibu wa masharti ya ibara hii ndogo kazi yoyote ya Rais aliyokabidhiwa na sheria yoyote inayotokana na masharti ya mkataba wowote uliotiwa sahihi na Jamhuri ya Muungano iwapo kisheria Rais haruhusiwi kuwakilisha kazi hiyo kwa mtu mwingine yoyote;

(b)ifahamike kwamba maagizo yanayotolewa na Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara hii ndogo, ya kumwagiza Waziri yeyote kutekeleza kazi yoyote ya Rais, hayatahesabiwa kwamba yanamzuia Rais kutekeleza kazi hiyo yeye mwenyewe.

(9)Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara hii-

(a)Mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanywa kwa ajili ya kuwasilisha kwa Jaji Mkuu azimio kuhusu hali ya afya ya Rais utahesabiwa kuwa ni mkutano halali hata kama mjumbe yeyote wa Baraza hilo hayupo au kiti chake ki wazi, na itahesabiwa kuwa Baraza limepitisha azimio hilo ikiwa litaungwa mkono kwa kauli ya wajumbe walio wengi waliohudhuria mkutano na kupiga kura.

(b)Rais hatahesabiwa kuwa hayupo katika Jamhuri ya Muungano kwa sababu tu ya kupitia nje ya Tanzania wakati yuko safarini kutoka sehemu moja ya Tanzania kwenda sehemu nyingine, au kwa sababu kwamba ametoa maagizo kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (7) na maagizo hayo bado hayajabatilishwa.

(10)Bila ya kujali masharti yaliyoelezwa hapo awali katika ibara hii, mtu atakayetekeleza kazi na shughuli za Rais, kwa mujibu wa ibara hii hatakuwa na madaraka ya kulivunja Bunge, kumwondoa yeyote kati ya Mawaziri katika madaraka yake au kufuta uteuzi wowote uliofanywa na Rais.

(11)Mtu yeyote atakayetekeleza kazi na shughuli za Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara hii kama ni Mbunge hatapoteza kiti chake katika Bunge wala hatapoteza sifa zake za kuchaguliwa kuwa Mbunge kwa sababu tu ya kutekeleza kazi na shughuli za Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara hii.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.9 Sheria ya 1992 Na.4 ib … Na.20 ib.12, Sheria yua 1994 Na.34 ib.6

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.