Ibara 130
Majukumu ya Tume na Taratibu za Utekelezaji
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Sekretariet ya Maadili ya Viongozi wa Umma · Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
(1)Tume ya Haki na Utawala Bora itatekeleza majukumu yafuatayo:
(a)kuhamasisha nchini hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi;
(b)kufanya shughuli za kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu kwa jumla;
(c)kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
(d)kufanya utafiti, kutoa na kueneza nchini elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora;
(e)kama ikibidi, kufungua mashauri mahakamani ili kuzuia vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu au kurekebisha haki inayotokana na uvunjwaji huo wa haki za binadamu, au ukiukwaji wa misingi ya utawala bora;
(f)kuchunguza mwenendo wa mtu yeyote anayehusika au taasisi yoyote inayohusika na masharti ya ibara hii katika utekelezaji wa kawaida wa madaraka ya kazi au majukumu yake au utekelezaji unaokiuka madaraka hayo;
(g)kutoa ushauri kwa Serikali na vyomno vingine vya umma na vya sekta ya binafsi kuhusu haki za binadamu na utawala bora;
(h)kuchukua hatua zipasazo kwa ajili ya kukuza na kuendeleza usuluhishi na suluhu miongoni mwa watu na taasisi mbalimbali wanaofika au kufikishwa mbele ya Tume.
(2)Tume itakuwa ni idara inayojitegemea, na bila ya kuathiri masharti meingine ya ibara hii, katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii, Tume haitalazimika kufuata maagizo au amri ya mtu yeyote au idara yoyote ya Serikali au maoni ya chama chochote cha siasa au ya taasisi nyingine yoyote ya umma au ya sekta ya binafsi.
(3)Masharti ya ibara ndogo ya (2) yasihesabiwe kuwa yanamzuia Rais kutoa maagizo au amri kwa Tume, wala hayatoi Haki kwa Tume kutofuata maagizo au amri, endapo Rais ataona kuwa, kuhusiana na jambo lolote au hali yoyote, masilahi ya taifa yahitajia hivyo.
(4)Tume itafanya uchunguzi kwa kufuata masharti ya ibara hii na masharti ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo, na itafanya uchunguzi juu ya mtu yeyote anayehusika au taasisi yoyote inayohusika kila itakapoagizwa na Rais kufanya uchunguzi; vilevile, isipokuwa kama Rais ameagiza Tume isifanye uchunguzi, Tume yaweza kufanya uchunguzi wakati wowote inapoona infaa kuchunguza mwenendo wa mtu yeyote anayehusika, au taasisi yoyote inayohusika, na masharti ya ibara hii anayetuhumiwa au inayotuhumiwa kwa kukiuka madaraka ya kazi yake, kutumia vibaya madaraka ya kazi yake au majukumu ya taasisi hiyo au kwa uvunjaji wa haki za binadamu au misingi ya utawala bora.
(5)Tume haitakuwa na mamlaka yoyote, ama kwa mujibu wa masharti ya ibara hii au masharti ya sheria yoyote iliyotungwa na Bunge kwa madhumuni ya sura hii ya Katiba hii ya kuchunguza uamuzi wa Jaji yeyote, Hakimu yeyote au wa Mahakama iwapo uamuzi huo ameutoa katika kutekeleza madaraka ya kazi yake; vile vile Tume haitakuwa na mamlaka ya kuchunguza uamuzi wowote uliotolewa na chombo chochote chenye asili ya Mahakama kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria iwapo uamuzi huo umetolewa katika kutekeleza mamlaka yake.
(6)Masharti ya ibara hii yatatumika kwa watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na wale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, watumishi na viongozi wa vyama vya siasa wanaoshughulikia mambo ya umma, wajumbe na watumishi wa Tume zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano na za Serikali hizo, mashirika ya umma na vyombo vingine vya umma au vya binafsi, kama ni kampuni, jumuiya, ushirika, wadhamini au muundo mwingine wowote, kadri itakavyoelezwa katika sheria iliyotungwa na Bunge; lakini masharti haya hayatatumika kwa Rais wala kwa Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar isipokuwa tu kwa kuzingatia masharti ya ibara ya 46 ya Katiba hii au ibara ya 36 ya Katiba ya Zanzibar, ya 1984.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 2000 Na.3 ib.17
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.