Ibara 131
Mamlaka ya Tume na utaratibu wa shughuli zake
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Sekretariet ya Maadili ya Viongozi wa Umma · Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
(1)Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya ibara hii, Bunge laweza kutunga sheria kwa mujibu wa masharti ya Sura hii ya Katiba hii kwa ajili ya kuweka masharti kuhusu mamlaka ya Tume, utaratibu wa kuendesha shughuli zake na kuhusu kinga za kisheria watakazokuwa nazo Makamishna na watumishi wa Tume kwa makusudi ya kuwawezesha kutekeleza kazi zao bila ya matatizo ya kisheria.
(2)Tume haitachunguza mambo yafuatayo, kwa madhumuni ya kutekeleza majukumu yake, yaani:
(a)jambo lolote ambalo liko mbele ya Mahakama au chombo kinginecho cha kimahakama;
(b)jambo lolote linalohusu uhusiano au mashirikiano kati ya Serikali na Serikali ya nchi yoyote ya nje au Shirika la Kimataifa;
(c)jambo linalohusu madaraka ya Rais kutoa msamaha;
(d)jambo jingine lolote lililotajwa na sheria yoyote.
(3)Kila mwaka wa fedha Tume itatayarisha na kuwasilisha kwa Waziri anayesimamia haki za binadamu taarifa kuhusu-
(a)shughuli za Tume katika mwaka uliotangulia;
(b)hali ya utekelezaji wa hifadhi ya haki za binadamu katika Jamhuri ya Muungano,
Na Waziri atawasilisha mbele ya Bunge kila taarifa iliyowasilishwa kwake na Tume mapema iwezekanavyo baada ya kuipokea.
(4)Masharti ya ibara ndogo ya (3) hayatahesabiwa kuwa yanaizuia Tume kuwasilisha taarifa nyingine yoyote kwa mtu mwingine au mamlaka nyingine yoyote.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 2000 Na.3 ib.17
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.