Ibara 132
Sekretarieti ya Maadili
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Sekretariet ya Maadili ya Viongozi wa Umma · Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
(1)Kutakuwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo itakuwa na mamlaka ya kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yanazingatiwa ipasavyo.
(2)Kwa madhumuni ya ibara hii, maana ya kiongozi wa umma na masharti ya maadili ya viongozi wa umma itabidi ifahamike kwa mujibu wa masharti ya sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma au masharti ya sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge kwa kadri masharti hayo yanavyohusika na suala la uongozi na ufafanuzi wake.
(3)Sekretarieti ya Maadili itakuwa na Kamishna wa Maadili na wafanya kazi wengine ambao idadi yao itatajwa na sheria iliyotungwa na Bunge.
(4)Bunge litatunga Sheria itakayoainisha misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma itakayozingatiwa na watu wote wanaoshika nafasi za madaraka zitakazotajwa na Bunge.
(5)Misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma:
(a)itafafanua nafasi za madaraka ambazo watu wenye kushika nafasi hizo watahusika nayo;
(b)itawataka watu wanaoshika nafasi fulani za madaraka kutoa mara kwa mara maelezo rasmi kuhusu mapato, rasilimali na madeni yao;
(c)itapiga marufuku mienendo na tabia inayopelekea kiongozi kuonekana hana uaminifu, anapendelea au si muadilifu au inaelekea kukuza au kuchochea rushwa katika shughuli za umma au inahatarisha maslahi au ustawi wa jamii;
(d)itafafanua adhabu zinazoweza kutolewa kwa kuvunja misingi ya maadili;
(e)itaelekeza taratibu, madaraka na desturi zitakazofuatwa ili kuhakikisha utekelezaji wa maadili;
(f)itaweka masharti mengine yoyote yanayofaa au ambayo ni muhimu kwa madhumuni ya kukuza na kudumisha uaminifu, uwazi, kutopendelea na uadilifu katika shughuli za umma na kwa ajili ya kulinda fedha na mali nyinginezo za umma.
(6)Bunge laweza kwa sheria kuweka masharti ya mtu kufukuzwa au kuondolewa kazini kutokana na kuvunja maadili ya viongozi, bila ya kujali kama kazi hiyo ni ya kuchaguliwa na kuteuliwa.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1995 Na.12 ib.18
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.