Wakili Msomi

Ibara 57

Wakati na muda wa Mawaziri kushika madaraka

Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Waziri Mkuu, Baraza la Mawaziri na Serikali

(1)Muda wa kushika madaraka ya Waziri na Naibu Waziri utaanza tarehe atakapoteuliwa kushika madaraka hayo.

(2)Kiti cha Waziri au Naibu Waziri kitakuwa wazi litokeapo lo lote kati ya mambo yafuatayo:-

(a)endapo mwenye madaraka atajiuzulu au kufariki dunia;

(b)ikiwa mwenye madaraka hayo atakoma kuwa Mbunge kwa sababu yoyote isiyohusika na kuvunjwa kwa Bunge;

(c)ikiwa Rais atafuta uteuzi na kumuondoa kazini mwenye madaraka hayo;

(d)iwapo atachaguliwa kuwa Spika;

(e)iwapo Waziri Mkuu atajiuzulu au kiti chake kikiwa wazi kwa sababu nyingine yoyote;

(f)ukiwadia wakati wa Rais mteule kushika madaraka ya Rais basi mara tu kabla Rais mteule hajashika madaraka hayo;

(g)iwapo Baraza la Maadili linatoa uamuzi unaothibitisha kwamba amevunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ibara 9 Sheria ya 1992 Na.20 ibara 9 Sheria ya 1992 Na.20 ibara 11 Sheria ya 1995 Na.12 ibara 8

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.