Wakili Msomi

Ibara 128

Utaratibu katika vikao vya Mahakama Maalum ya Katiba

Utoaji Haki katika Jamhuri ya Muungano, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Tume ya Kuajiri ya Mahakama ya Tanzania Bara, Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano · Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano

(1)Mahakama Maalum ya Katiba itafanya vikao vyake wakati ule tu kunapokuwa na shauri la kusikiliza, na itafanya vikao vyake mahali popote patakapoamuliwa kwa utaratibu utakaotumika kwa ajili ya mashauri yatakayosikilizwa na Mahakama Maalum ya Katiba.

(2)Kiwango cha kila kikao cha Mahakama Maalum ya Katiba ni wajumbe wote, na iwapo mjumbe yeyote atakuwa hayupo au ikiwa kiti cha mjumbe yoyote kitakuwa wazi basi Serikali iliyomteua mjumbe huyo ambaye hayupo au ambaye kiti chake ki wazi itamteua mjumbe mwingine wa kushika mahali pake. Mjumbe wa muda aliyeteuliwa kwa mujibu wa ibara hii ndogo ataendelea kutekeleza kazi katika Mahakama Maalum ya Katiba mpaka mjumbe wa kawaida atakaporejea kazini au mpaka mtu atakapoteuliwa kujaza nafasi iliyo wazi au mpaka shauri litakapokwisha, kutegemea ni lipi kati ya mambo hayo litakalotokea mapema zaidi.

(3)Kila suala linalohitaji uamuzi wa Mahakama Maalum ya Katiba litaamuliwa kwa kufuata kauli ya theluthi mbili ya wajumeb kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Zanzibar.

(4)Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti kuhusu utaratibu wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mahakama Maalum ya Katiba, utartibu wa kupeleka shauri mbele ya Mahakama hiyo, utaratibu wa kuendesha shauri katika Mahakama na utaratibu wa kuwasilisha Serikalini uamuzi wa Mahakama Maalum ya Katiba:

Isipokuwa kwamba iwapo shauri lolote litafikishwa mbele ya Mahakama Maalum ya Katiba wakati hakuna sheria yoyote ya aina iliyoelezwa katika ibara hii ndogo, basi shauri litasikilizwa na kuamuliwa kwa kufuata utaratibu utakaowekwa na Mahakama yenyewe kabla ya kuanza kusikiliza shauri, au iwapo Wajumbe wa Mahakama watashindwa kukubaliana juu ya utaratibu huo, basi shauri litasikilizwa na kuamuliwa kwa kufuata utaratibu utakaoamuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.37

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.