Ibara 129
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Sekretariet ya Maadili ya Viongozi wa Umma · Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
(1)Kutakuwa na Tume itakayoitwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambayo majukumu yake yatakuwa kama ilivyoelezwa katika ibara ya 130 ya Katiba hii.
(2)Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora itakuwa na Makamishna wafuatao:
(a)Mwenyekiti, ambaye atakuwa ni mtu mwenye sifa ya kuweza kuteuliwa kuwa Jaji;
(b)Makamu Mwenyekiti, ambaye atateuliwa kwa kuzingatia kanuni kwamba endapo Mwenyekiti ni mtu anayetoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, yeye atakuwa ni mtu wa kutoka upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano;
(c)Makamishna wengine wasiozidi watano watakaoteuliwa kutoka miongoni mwa watu wenye ujuzi, uzoefu na upeo mkubwa katika mambo ya haki za binadamu, sheria, utawala, siasa au mambo ya jamii;
(d)Makamishna Wasaidizi.
(3)Makamishna na Makamishna Wasaidizi wote watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Kamati ya Uteuzi.
(4)Kutakuwa na Kamati ya Uteuzi kwa madhumuni ya ibara hii ambayo itakuwa na wajumbe wafuatao:
(a)Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani;
(b)Spika wa Bunge;
(c)Jaji Mkuu wa Zanzibar;
(d)Spika wa Baraza la Wawakilishi; na
(e)Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye atakuwa ndiye Katibu wa Kamati hii.
(5)Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna wengine wote kila mmoja atashika madaraka yake kwa kipindi cha miaka mitatu na anaweza kuteuliwa tena kwa kipindi kingine kimoja tu cha miaka mitatu.
(6)Kwa madhumuni ya kuwakinga Makamishna kutokana na migongano ya kimasilahi, mtu yeyote akiteuliwa kuwa Kamishna wa Tume atalazimika kuacha mara moja madaraka yoyote katika chama chochote cha siasa au madaraka ya aina nyingine yoyote itakayotajwa kwa ajili hiyo na sheria iliyotungwa na Bunge.
(7)Kamishna au Kamishna Msaidizi wa Tume aweza tu kuondolewa katika madaraka ya kazi yake katika Tume kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi yake, ama kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote, au kwa sababu ya tabia mbaya inayoathiri maadili ya kazi ya Kamishna.
(8)Tume yaweza kutekeleza shughuli zake bila ya kujali kwamba kuna nafasi iliyo wazi miongoni mwa viti vya wajumbe au kwamba mjumbe mmojawapo hayupo.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 2000 Na.3 ib.17
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.