Ibara 59
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano
Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Waziri Mkuu, Baraza la Mawaziri na Serikali
(1)Kutakuwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambaye katika ibara zifuatazo za Katiba hii atatajwa tu kwa kifupi kama "Mwanasheria Mkuu" ambaye atateuliwa na Rais.
(2)Mtu yeyote hatastahili kuteuliwa kushika madaraka ya Mwanasheria Mkuu isipokuwa tu kama kwa mujibu wa Katiba hii ana sifa maalum, kama ilivyofafanuliwa katika ibara ya 109(8) zinazomwezesha kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano au Jaji wa Mahakam Kuu ya Zanzibar, na amekuwa na mojawapo ya hizo sifa maalum kwa muda usiopungua miaka mitano.
(3)Mwanasheria Mkuu atakuwa ndiye mshauri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo ya sheria na, kwa ajili hiyo, atawajibika kutoa ushauri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusu mambo yote ya kisheria, na kutekeleza shughuli nyinginezo zozote zenye asili ya au kuhusiana na sheria zitakazopelekwa kwake au atakazoagizwa na Rais kuzitekeleza, na pia kutekeleza kazi au shughuli nyinginezo zilizokabidhiwa kwake na Katiba hii au na sheria yoyote.
(4)Katika kutekeleza kazi na shughuli zake kwa mujibu wa ibara hii, Mwanasheria Mkuu atakuwa na haki ya kuhudhuria na kusikilizwa katika Mahakama zote katika Jamhuri ya Muungano.
(5)Mwanasheria Mkuu atakuwa Mbunge kutokana na wadhifa wake, na atashika madaraka yake mpaka-
(a)uteuzi wake utakapofutwa na Rais au
(b)mara tu kabla ya Rais mteule kushika madaraka ya Rais, na atalipwa mshahara, posho na malipo mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ibara 9 Sheria ya 1992 Na.4 ibara 16
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.