Wakili Msomi

Ibara 109

Majaji wa Mahakama Kuu na uteuzi wao

Utoaji Haki katika Jamhuri ya Muungano, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Tume ya Kuajiri ya Mahakama ya Tanzania Bara, Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano · Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano

(1)Kutakuwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu (ambaye katika ibara zifuatzo kwenye Katiba Hii atatajwa tu kwa kifupi kama "Jaji Kiongozi") na Majaji wengine wa Mahakama Kuu wasiopungua kumi na watano.

(2)Jaji Kiongozi na Majaji wengineo wa Mahakama Kuu watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Tume ya Kuajiri ya Mahakama.

(3)Bila ya kuathiri masharti ya Katiba hii au sheria nyingine yoyote kuhusu madaraka ya Jaji Mkuu aliyetajwa katika ibara ya 118, Jaji Kiongozi atakuwa ndiye msaidizi maalum wa Jaji Mkuu katika utendaji wa kazi katika Mahakama Kuu na Mahakama nyinginezo zote za ngazi ya chini yake, na katika madaraka hayo Jaji Kiongozi atatekeleza kazi na shughuli atakazoagizwa au kuelekezwa mara kwa mara na Jaji Mkuu, na kwa madhumuni ya ibara hii, Jaji Kiongozi atajulikana pia kama Mkuu wa Mahakama Kuu.

(4)Mbali ya madaraka yake ya kawaida ya Jaji wa Mahakama Kuu kama Majaji wengine wote wa Mahakama Kuu, Jaji Kiongozi atakuwa pia na mamlaka ya kutekeleza kazi na shughuli zote zinazoambatana na mamlaka ya Mahakama Kuu ambazo kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au ya sheria nyingine yoyote au kufuatana na mila za kisheria zinazotumika hutakiwa zitekelezwe na Mkuu wa Mahakama Kuu:

Isipokuwa kwamba masharti ya ibara hii ndogo hayatatumika kwa ajili ya utekelezaji wa kazi au shughuli ambazo kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au ya Sheria nyingine yoyote au kufuatana na mila za kisheria zinazotumika Tanzania zimetajwa mahususi au zinafahamika kuwa ni kazi au shughuli zinazotakiwa kutekelezwa tu na Jaji Mkuu.

(5)Kwa madhumuni ya kuondoa mashaka juu ya ufafanuzi au utekelezaji wa masharti ya ibara ndogo ya (3) na ya (4) ya ibara hii, inatamkwa rasmi hapa kwamba isipokuwa kama masharti ya Katiba hii au ya sheria nyingine yoyote yameagiza vingine, Jaji Mkuu atakuwa na uwezo wa kutoa kwa Jaji Kiongozi mara kwa mara maagizo au maelekezo kuhusu utendaji wa kazi na shughuli zake kama Mkuu wa Mahakama Kuu: vile vile, Jaji Mkuu atakuwa na uwezo wa kuwakilisha kwa Jaji Kiongozi baadhi ya madaraka yake ya uongozi na usimamizi juu ya utekelezaji wa kazi katika Mahakama Kuu na Mahakama nyinginezo zote za ngazi ya chini yake, na kila inapohitajika, Jaji Mkuu anaweza kutekeleza yeye mwenyewe moja kwa moja madaraka yake yoyote aliyowakilisha kwa Jaji Kiongozi.

(6)Kazi ya Jaji wa Mahakama Kuu haitafutwa wakati yupo mtu aliyeshika madaraka ya kiti cha Jaji.

(7)Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (9) ya ibara hii, mtu aweza tu kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ikiwa ana sifa maalum, kama ilivyofafanuliwa katika ibara ndogo ya (8) ya ibara hii, na awe mtu ambaye amekuwa na mojawapo ya sifa maalum kwa muda usiopungua miaka mitano.

(8)Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa ibara ndogo ya (7), ya (9) na ya (11) ya ibara hii, "sifa maalum" maana yake ni sifa zilizotajwa katika Sheria ya Mawakili (au Sheria nyingine yoyote inayobadilisha hiyo sheria ya Mawakili au inayotumika badala yake) ambazo ni lazima mtu awe nazo mojawapo ya sifa hizo ili aweze kukubaliwa kuandikishwa kama Wakili Tanzania Bara.

(9)Iwapo Rais atatosheka kwamba ijapokuwa mtu mwenye sifa mojawapo ya hizo sifa maalum hakuwa nayo sifa hiyo kwa muda usiopungua miaka mitano, lakini mtu huyo ana uwezo, ujuzi na kwa kila hali anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu na kuna sababu za kumfanya mtu huyo astahili kukabidhiwa madaraka hayo, basi Rais aweza kutangua lile sharti la kuwa na sifa maalum kwa muda usiopungua miaka mitano, na baada ya kushauriana na Tume ya Kuajiri ya Mahakama, Rais aweza kumteua mtu huyo kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

(10)Ikitokea kwamba kiti cha Jaji Kiongozi kitakuwa wazi au kwamba Jaji Kiongozi atashindwa kutekeleza kazi zake kwa sababu yoyote, basi kazi hizo zitatekelezwa na Jaji mmojwapo atakayeteuliwa na Rais kwa ajili hiyo, na na Jaji huyo atatekeleza kazi hizo mpaka atakapoteuliwa Jaji Kiongozi mwingine na kushika madaraka ya kiti cha Jaji Kiongozi au mpaka Jaji Kiongozi mwenyewe ambaye alikuwa hamudu kazi zake atakaporejea kazini.

(11)Ikitokea kwamba kiti cha Jaji yeyote kitakuwa wazi au ikiwa Jaji yeyote atateuliwa kuwa Kaimu Jaji Kiongozi au kama atashindwa kutekeleza kazi zake kwa sababu yoyote, au kama Jaji Mkuu atamshauri Rais kuwa kazi za Mahakama Kuu zilivyo wakati huo zahitaji ateuliwe Kaimu Jaji, basi Rais aweza, baada ya kushauriana na Jaji Mkuu kama kawaida, kuteua Kaimu Jaji kutoka miongoni mwa watu wenye sifa maalum.

Isipokuwa kwamba

(a)mtu hatahesabiwa kuwa hastahili kuteuliwa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii ndogo kwa sababu tu kwamba ametimiza umri uliotajwa katika ibara ndogo ya (1) ya ibara ya 61 ya Katiba hii;

(b)kwa madhumuni ya kumteua Kaimu Jaji kwa mujibu wa masharti ya ibara hii ndogo, Rais aweza kutangua lile sharti la kuwa na sifa maalum kwa muda usiopungua miaka mitano kwa sababu kama zile zilizotajwa katika ibara ndogo ya (9) ya ibara hii.

(12)Mtu yeyote atakayeteuliwa kuwa Kaimu Jaji kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (11) ya ibara hii, ataendelea kufanya kazi kama Kaimu Jaji kwa muda wowote utakaotajwa wakati wa kuteuliwa kwake au, kama muda haukutajwa, mpaka uteuzi wake utakapofutwa na Rais, lakini bila ya kujali kwamba muda wake wa kazi umemalizika au kwamba uteuzi wake umefutwa, mtu huyo aweza kuendelea kufanya kazi kama Kaimu Jaji mpaka amalize kutayarisha na kutoa hukumu au mpaka akamilishe shughuli nyingine yoyote inayohusika na mashauri ambayo alikwisha anza kuyasiliza kabla ya muda wake wa kazi haujamalizika au kabla ya uteuzi wake haujafutwa.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1979 Na.14 ib.6 1985 Sheria ya 1985 Na.15 ib.22 Sheria ya 1990 Na.14 ib.5

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.