Wakili Msomi

Ibara 110

Muda wa Majaji wa Mahakama Kuu kushika madaraka

Utoaji Haki katika Jamhuri ya Muungano, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Tume ya Kuajiri ya Mahakama ya Tanzania Bara, Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano · Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano

(1)Kila Jaji wa Mahakama Kuu atalazimika kuacha kazi yake atakapotimiza umri wa miaka sitini lakini masharti ya ibara hii ndogo yatatumika bila ya kuathiri masharti yafuatayo katika ibara hii.

(2)Jaji yeyote wa Mahakama Kuu aweza kujiuzulu kazi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wakati wowote baada ya kutimia umri wa miaka hamsini na tano, isipokuwa kama Rais ataagiza kwamba asijiuzulu, na iwapo Rais ataagiza hivyo, basi huyo Jaji atakayehusika na maagizo hayo ya Rais hatakuwa na haki ya kujiuzulu mpaka upite kwanza muda wowote utakaotajwa na Rais kwa ajili hiyo.

(3)Iwapo Rais ataona kuwa kwa ajili ya manufaa ya Umma inafaa Jaji aliyetimiza umri wa miaka sitini aendelee kufanya kazi, na huyo Jaji mwenyewe anakubali kwa maandishi kuendelea kufanya kazi, basi Rais aweza kuagiza kuwa Jaji huyo aendelee kufanya kazi kwa muda wowote utakaotajwa na Rais.

(4)Bila ya kujali kwamba Jaji ametimiza umri ambao analazimika kuacha kazi kwa mujibu wa masharti ya ibara hii, mtu anayefanya kazi ya Jaji wa Mahakama Kuu aweza kuendelea kufanya kazi baada ya kutimiza umri huo mpaka amalize kutayarisha na kutoa hukumu au mpaka akamilishe shughuli nyingine yoyote inayohusika na mashauri ambayo alikwisha anza kuyasikiliza kabla hajatimiza umri huo wa kuacha kazi.

(5)Jaji wa Mahakama Kuu aweza tu kuondolewa katika madaraka ya kazi ya kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi yake (ama kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote) au kwa sababu ya tabia mbaya inayoathiri maadili ya kazi ya Jaji au sheria ya maadili ya viongozi wa umma; na hataweza kuondolewa kazini ila kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (7) ya ibara hii.

(6)Iwapo Rais anaona kuwa suala la kumwondoa Jaji kazini lahitaji kuchunguzwa, basi katika hali hiyo mambo yatakuwa ifuatavyo:-

(a)Rais atateua Tume ambayo itakuwa na Mwenyekiti na Wajumbe wengine wasiopungua wawili. Na huyo Mwenyekiti na angalau nusu ya Wajumbe wengine wa Tume hiyo itabidi wawe watu ambao ni Majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani katika nchi yoyote iliyomo kwenye Jumuiya ya Madola.

(b)Tume hiyo itachunguza shauri lote halafu itatoa taarifa kwa Rais kuhusu maelezo ya shauri lolote na itamshauri Rais kama huyo Jaji anayehusika aondolewe kazini kwa mujibu wa masharti ya ibara hii kwa sababu ya kushindwa kufanya kazi kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote au kwa sababu ya tabia mbaya.

(7)Ikiwa Tume iliyoteuliwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (6) itamshauri Rais kwamba jaji ambaye habari zake zimechunguzwa na hiyo Tume aondolewe kazini kwa sababu ya kushindwa kufanya kazi kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyte au kwa sababu ya tabia mbaya, basi Rais atamwondoa kazini Jaji huyo anayehusika.

(8)Ikiwa suala la kumwondoa Jaji kazini limepelekwa kwenye Tume kwa ajili ya uchunguzi kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (6) ya ibara hii, Rais aweza kumsimamisha kazi Jaji huyo anayehusika, na Rais aweza wakati wowote kufuta uamuzi huo wa kumsimamisha kazi Jaji huyo, na kwa hali yoyote uamuzi huo utabatilika ikiwa Tume itamshauri Rais kwamba jaji huyo asiondolewe kazini.

(9)Masharti ya ibara hii yatatumika bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (12) ya ibara ya 109 ya Katiba hii.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1979 Na.14 ib.6: na Sheria ya 1985 Na.15 ib.22 na 23 Sheria ya 1995 Na.12 ib.17

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.