Ibara 120
Muda wa Majaji wa Mahakama ya Rufani kushika madaraka
Utoaji Haki katika Jamhuri ya Muungano, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Tume ya Kuajiri ya Mahakama ya Tanzania Bara, Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano · Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano
(1)Kila Jaji wa Mahakama ya Rufani atalazimika kuacha kazi yake atakapotimiza umri wa miaka sitini na tano, lakini masharti ya ibara hii ndogo yatatumika bila kuathiri masharti yafuatayo katika ibara hii.
(2)Jaji yeyote wa Mahakama ya Rufani aweza kujiuzulu kazi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wakati wowote baada ya kutimiza umri wa miaka sitini, isipokuwa kama Rais ataagiza kwamba asijiuzulu, na iwapo Rais ataagiza hivyo, basi huyo Jaji wa Mahakama ya Rufani atakayehusika na maagizo hayo ya Rais hatakuwa na haki ya kujiuzulu mpaka upite kwanza muda wowote utakaotajwa na Rais kwa ajili hiyo.
(3)Iwapo Rais ataona kuwa kwa ajili ya manufaa ya Umma inafaa Jaji wa Mahakama ya Rufani aliyetimiza umri wa miaka sitini na tano aendelee kufanya kazi, na huyo Jaji mwenyewe wa Mahakama ya Rufani anakubali kwa maandishi kuendelea kufanya kazi; basi Rais aweza kuagiza kuwa Jaji huyo wa Mahakama ya Rufani aendelee kufanya kazi kwa muda wowote utakaotajwa na Rais.
(4)Bila ya kujali kwamba Jaji wa Mahakama ya Rufani ametimiza umri ambao analazimika kuacha kazi kwa mujibu wa masharti ya ibara hii, mtu anayefanya kazi ya Jaji wa Mahakama ya Rufani aweza kuendelea kufanya kazi baada ya kutimiza umri huo mpaka amalize kutayarisha na kutoa hukumu au mpaka akamilishe shughuli nyingine yoyote inayohusika na mashauri ambayo alikwisha anza kuyasikiliza kabla hajatimiza umri huo wa kuacha kazi.
(5)Jaji wa Mahakama ya Rufani aweza tu kuondolewa katika madaraka ya kazi ya Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake (ama kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote) au kwa sababu ya tabia mbaya, na hataweza kuondolewa kazini ila kwa mujibu wa masharti ya utaratibu unaofanana na ule uliowekwa kwa ajili ya kumwondoa kazini Jaji wa Mahakama Kuu kama ilivyoelezwa katika ibara ndogo ya (6) na ya (7) ya ibara ya 110 ya Katiba hii, na kwa ajili hiyo masharti ya ibara ndogo ya (8) ya ibara hiyo ya 110 yatatumika kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa namna ile ile yanavyotumika kwa Jaji wa Mahakama Kuu.
(6)Masharti ya ibara hii yatatumika bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (5) ya ibara ya 118 ya Katiba hii.
Marejeo ya marekebisho: sheria za 1979 Na.14 ib.8 na Sheria ya 1984 Na.15 ib.30
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.