Wakili Msomi

Ibara 118

Majaji wa Mahakama ya Rufani na uteuzi wao

Utoaji Haki katika Jamhuri ya Muungano, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Tume ya Kuajiri ya Mahakama ya Tanzania Bara, Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano · Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano

(1)Kutakuwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani (ambaye katika ibara zifuatazo kwenye Katiba hii atatajwa tu kwa kifupi kama "Jaji Mkuu" na Majaji wengine wa Mahakama ya Rufani wasiopungua wawili, isipokuwa kwamba kikao maalum cha Mahakama nzima kitakuwa kamili kikiwa na Majaji wa Rufani wasiopungua watano.

(2)Jaji Mkuu atateuliwa na Rais na atakuwa ndiye Kiongozi wa Mahakama ya Rufani na pia Mkuu wa Idara ya Mahakama kama ilivyofafanuliwa katika ibara ya 116 ya Katiba hii.

(3)Majaji wengineo wa Mahakama ya Rufani watateuliwa na Rais, baada ya kushauriana na Jaji Mkuu, kutoka miongoni mwa watu ambao wanaweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyoelezwa katika ibara ya 109 ya Katiba hii au kutoka miongoni mwa watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mujibu wa Sheria zinazotumika Zanzibar.

(4)Iwapo itatokea kwamba:-

(a)Kiti cha Jaji Mkuu kitakuwa wazi; au

(b)Jaji Mkuu hayupo Tanzania; au

(c)Jaji Mkuu atashindwa kutekeleza kazi yake kwa sababu yoyote na Rais akiona kuwa kwa muda wa tukio lolote kati ya hayo matatu inafaa kumteua Kaimu Jaji Mkuu, basi Rais aweza kumteua Kaimu Jaji Mkuu kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kustahili kuteuliwa kuwa Majaji wa Mhakama ya Rufani, na huyo Kaimu Jaji Mkuu atatekeleza kazi za Jaji Mkuu mpaka atakapoteuliwa Jaji Mkuu au mpaka Jaji Mkuu mwingine ambaye alikuwa hayupo Tanzania au alikuwa hamudu kazi zake atakaporejea kazini.

(5)Ikitokea kwamba kiti cha Jaji yeyote wa Mahakama ya Rufani kitakuw wazi au ikiwa Jaji yeyote wa Mahakama ya Rufani atateuliwa kuwa Kaimu Jaji Mkuu au kama atashindwa kutekeleza kazi zake kwa sababu yoyote, au Jaji Mkuu atamshauri Rais kuwa kazi za Mahakama kama ya Rufani ilivyo wakati huo zahitaji ateuliwe Kaimu Jaji wa Mahakama ya Rufani, basi Rais aweza, baada ya kushauriana na Jaji Mkuu kama kawaida, kumteua Kaimu Jaji wa Mahakama ya Rufani kutoka miongoni mwa watu ambao wanaweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (3) ya ibara hii.

(6)Mtu yeyote atakayeteuliwa kuwa Kaimu Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (5) ya ibara hii, ataendelea kufanya kazi kama Kaimu Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa muda wowote utakaotajwa wakati wa kuteuliwa kwake, au, kama muda haukutajwa, mpaka uteuzi wake utakapofutwa na Rais, lakini bila ya kujali kwamba muda wake wa kazi umemalizika au kwamba uteuzi wake umefutwa, mtu huyo aweza kuendelea kufanya kazi kama Kaimu Jaji wa Mahakama ya Rufani mpaka amalize kutayarisha na kutoa hukumu au mpaka akamilishe shughuli nyingine yoyote inayohusika na rufaa au mashauri mengine yoyote ambayo alikwisha anza kuyasikiliza kabla muda wake wa kazi haujamalizika au kabla ya uteuzi wake haujafutwa.

(7)Kwa madhumuni ya kuondoa mashaka juu ya ufafanuzi wa masharti ya ibara ndogo ya (1) ya ibara ya 118 ya Katiba hii (inayotaja idadi ya Majaji wa kudumu wa Mahakama ya Rufani) na masharti ya ibara ya 119 ya Katiba hii (inayoeleza mamlaka ya Majaji wa Mahakama ya Rufani), inatamkwa rasmi hapa kwamba Kaimu Jaji wa Mahakama ya Rufani aliyeteuliwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (5) ya ibara hii, atakuwa na mamlaka kamili ya Jaji wa Mahakama ya Rufani na kwamb atatekeleza kazi zake kama Kaimu Jaji wa Mahakama ya Rufani bila ya kujali kuwa kuteuliwa kwake kutakiuka idadi ya Majaji wa kudumu wa Mahakama ya Rufani iliyotajwa katika ibara ndogo ya (1) ya ibara 118 ya Katiba hii, lakini masharti ya ibara hii ndogo yatatumika bila ya kuathiri masharti ya ibara ya 122 ya Katiba hii kuhusu kiwango cha vikao vya Mahakama ya Rufani.

(8)Kazi ya Jaji wa Mahakama ya Rufani haitafutwa wakati yupo mtu aliyeshika madaraka ya kiti cha Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Marejeo ya marekebisho: Sheria za 1979 Na.14 ib.8 na Sheria ya 1984 Na.15 ib.28

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.