Ibara 116
Tafsiri
Utoaji Haki katika Jamhuri ya Muungano, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Tume ya Kuajiri ya Mahakama ya Tanzania Bara, Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano · Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano
(1)Katika Sehemu hii ya Tano ya Sura hii ya Tano ya Katiba hii na katika sehemu nyingine za Katiba hii, ila iwapo maelezo yahitaji vinginevyo: "Idara ya Mahakama" maana yake ni Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano iliyotajwa katika ibara ya 117 ya Katiba hii (au kwa kifupi "Mahakama ya Rufani"), Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano iliyotajwa katika ibara ya 108 ya Katiba hii (ambayo itajulikana kwa kifupi kama "Mahakama Kuu) pamoja na Mahakama nyingine zozote za ngazi zilizo chini ya Mahakama Kuu; "Jaji Mkuu" maana yake ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani na ni pamoja na Kaimu Jaji Mkuu au Jaji wa Rufani anayeshikilia au kutekeleza madaraka ya Jaji Mkuu; "Jaji wa Rufani" maana yake ni Jaji yoyote wa Mahakama ya Rufani.
(2)Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (3), Jaji Mkuu hatakuwa na madaraka juu ya jambo lolote linalohusu muundo na uendeshaji wa shughuli za siku hadi siku za Mahakama zilizoundwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar au sheria yoyote ya Tanzania Zanzibar.
(3)Jaji Mkuu atashauriana mara kwa mara na Jaji Mkuu wa Zanzibar kuhusu uendeshaji wa shughuli za Mahakama ya Rufani kwa jumla, na pia kuhusu uteuzi wa Majaji wa Rufani.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.25 na 26
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.