Ibara 117
Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na Madaraka yake
Utoaji Haki katika Jamhuri ya Muungano, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Tume ya Kuajiri ya Mahakama ya Tanzania Bara, Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano · Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano
(1)Kutakuwa na Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano (itakayojulikana kwa kifupi kama "Mahakama ya Rufani") ambayo mamlaka yake yatakuwa kama ilivyoelezwa katika Katiba hii au katika Sheria nyingine yoyote.
(2)Mahakama ya Rufani haitakuwa na mamlaka yoyote kuhusu usuluhishi wa suala lolote litakaloshughulikiwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 126 ya Katiba hii ambayo inahusu ubishi kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
(3)Kazi ya Mahakama ya Rufani itakuwa ni kusikiliza na kutoa uamuzi juu ya kila rufaa inayoletwa mbele ya Mahakama ya Rufani kutokana na hukumu au uamuzi wa namna nyingine yoyote wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Hakimu.
(4)Sheria iliyotungwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na Bunge au na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar yaweza kuweka masharti yatakayoeleza utaratibu wa kupeleka rufaa mbele ya Mahakama ya Rufani, nyakati na sababu za kukata rufaa na namna ya kushughulikia rufaa hizo.
Marejeo ya marekebisho: sheria za 1979 Na.14 ib.8 na Sheria ya 1984 Na.15 ib.27
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.