Ibara 50
Muda wa Makamu wa Rais kushika Madaraka
Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Makamu wa Rais
(1)Isipokuwa kama atajiuzulu au atafariki mapema zaidi, mtu aliyechaguliwa, au kuteuliwa kwa mujibu wa ibara ya 37(5), kuwa Makamu wa Rais, bila ya kuathiri masharti mengine ya ibara hii, atashika kiti cha Makamu wa Rais kwa muda wa miaka mitano tangu alipochaguliwa kuwa Makamu wa Rais.
(2)Makamu wa Rais atashika kiti hicho hadi-
(a)muda wake utakapokwisha;
(b)akifariki dunia akiwa katika madaraka;
(c)atakapojiuzulu;
(d)atakapoapishwa kuwa Rais baada ya kiti cha Rais kuwa wazi;
(e)atakapotiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai linaloonyesha utovu wake wa uaminifu;
(f)atakapoapishwa Rais mwingine kushika nafasi ya Rais pamoja na Makamu wake;
(g)atakapoondolewa madarakani baada ya kushtakiwa Bungeni kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya
(3)ya ibara hii;
(h)atakapoacha kushika kiti cha Makamu wa Rais vinginevyo kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.
(3)Bunge litakuwa na madaraka ya kumuondoa Makamu wa Rais madarakani kama yale liliyonayo kuhusiana na Rais, isipokuwa kwamba hoja yoyote ya kumshtaki Makamu wa Rais itatolewa tu kama inadaiwa kwamba:-
(a)Rais amewasilisha hati ya Spika inayoeleza kwamba Makamu wa Rais ameacha au ameshindwa kutekeleza kazi za Makamu wa Rais;
(b)ametenda vitendo ambavyo kwa jumla vinaivunja Katiba au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;
(c)ametenda vitendo ambavyo vinakiuka maadili yanayohusu uandikishwaji wa vyama vya siasa yaliyotajwa katika ibara ya 20(2) ya Katiba; au
(d)amekuwa na mwenendo unaodhalilisha kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano au kiti cha Makamu wa Rais, na haitatolewa hoja ya namna hiyo ndani ya miezi kumi na miwili tangu hoja hiyo ilipotolewa na ikakataliwa na Bunge.
(4)Ikitokea kwamba kiti cha Makamu wa Rais ki wazi kutokana na masharti yaliyomo katika ibara ya 50(3), kifo au kujiuzulu basi mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote ndani ya siku zisizozidi kumi na nne baada ya kushika madaraka yake, Rais atamteua mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura za Wabunge walio wengi.
(5)Masharti mengine yote ya ibara ya 46A ya Katiba yatatumika pia kuhusiana na Makamu wa Rais isipokuwa tu kwamba Makamu wa Rais aliyeondolewa tena madarakani chini ya ibara ndogo ya (3) hatakuwa na sifa tena za kushika nafasi ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wala Rais wa Zanzibar.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1994 Ibara 11. Sheria ya 1995 Na.12 ibara 6 Sheria ya 2000 Na.3 ib.10
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.