Ibara 42
Wakati na muda wa kushika madaraka ya Rais
Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Rais
(1)Rais mteule atashika madaraka ya Rais mapema iwezekanavyo baada ya kutangazwa kwamba amechaguliwa kuwa Rais, lakini kwa hali yoyote itabidi ashike madaraka kabla ya kupita siku saba.
(2)Isipokuwa kama atajiuzulu au atafariki mapema zaidi mtu aliyechaguliwa kuwa Rais, bila ya kuathiri masharti yaliyo katika ibara ndogo ya (3), atashika kiti cha Rais kwa muda wa miaka mitano tangu siku alipochaguliwa kuwa Rais.
(3)Mtu aliyechaguliwa kuwa Rais atashika kiti cha Rais hadi-
(a)siku ambapo mtu atakayemfuatia katika kushika kiti hicho atakula kiapo cha Rais; au
(b)siku ambapo atafariki dunia akiwa katika madaraka; au
(c)siku atakapojiuzulu; au
(d)atakapoacha kushika kiti cha Rais kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.
(4)Iwapo Jamhuri ya Muungano inapigana vita dhidi ya adui na Rais anaona kuwa haiwezekani kufanya uchaguzi, Bunge laweza mara kwa mara kupitisha azimio la kuongeza muda wa miaka mitano uliotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara hii isipokuwa kwamba muda wowote utakaoongezwa kila mara hautazidi miezi sita.
(5)Kila Rais mteule na kila mtu atakayeshikilia kiti cha Rais, kabla ya kushika madaraka ya Rais, ataapa mbele ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, kiapo cha uaminifu na kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.9
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.