Ibara 151
Ufafanuzi
Mengineyo
(1)Katika Katiba hii, ila iwapo maelezo yahitaji vinginevyo: "amri ya Jeshi" maana yake ni sheria au amri iliyotolewa kwa mujibu wa sheria, ya kusimamia nidhamu katika jeshi; "askari" likitumika kuhusiana na jeshi lolote, maana yake ni pamoja na askari yeyote ambaye kwa mujibu wa amri ya jeshi hilo ni mtu anayewajibika kinidhamu; "Baraza la Wawakilishi" maana yake ni Baraza la Wawakilishi, la Zanzibar lililotajwa katika ibara ya 106 ya Katiba hii na linalotekeleza madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii na Katiba ya Zanzibar 1984; "Bunge" maana yake ni bunge la Jamhuri ya Muungano lililotajwa katika ibara ya 62 ya Katiba hii; "Chama cha Siasa" maana yake ni chama cha Siasa kilichoandikishwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria ya Vyama vya Siasa, ya Mwaka 1992;
"Idara ya Mahakama" maana yake ni kama ilivyofafanuliwa katika ibara ndogo ya (1) ya ibara ya 116 ya Katiba hii; "Idara ya Mahakama ya Zanzibar" maana yake ni Idara ya Mahakama inayojumlisha mahakama zote ambazo ziko katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; "Jaji Mkuu" maana yake ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani aliyetajwa katika ibara ndogo ya (1) ya ibara ya 115 ya Katiba hii ambaye ameteuliwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hiyo ya 118 au iwapo Jaji Mkuu hayupo au anashindwa kutekeleza kazi zake kwa sababu yoyote, Kaimu Jaji Mkuu aliyeteuliwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (4) ya ibara hiyo ya 118 ya Katiba hii, na kama Kaimu Jaji Mkuu naye hayupo au anashindwa kutekeleza kazi za Jaji Mkuu, Jaji wa Mahakama ya Rufani iliyepo kazini kwa wakati huo na ambaye yuko kwenye daraja la juu zaidi la madaraka kupita majaji wote wa Rufani waliopo; "Jaji Mkuu wa Zanzibar" maana yake ni Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar ambaye, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar 1984, ndiye Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Zanzibar; "Jeshi" maana yake ni lolote kati ya majeshi ya ulinzi na ni pamoja na jeshi lolote jingine lililoundwa na Katiba hii au kwa mujibu wa sheria na linalotawaliwa kwa amri ya jeshi; "Jumuiya ya Madola" maana yake ni jumuiya ambayo wanachama wake ni Jamhuri ya Muungano na kila nchi ambayo inahusika na masharti ya ibara ya 7 ya Sheria ya Uraia, ya mwaka 1961; "kiapo" maana yake itabidi ifahamike kwa maana ya kawaida ya neno hilo na ni pamoja na tamko rasmi la namna yoyote linaloruhusiwa kisheria kutumiwa badala ya kiapo; "kiapo cha uaminifu" maana yake ni kiapo cha kuwa mwaminifu kwa nchi na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano; "Maadili ya Kazi ya Jaji" maana yake ni masharti ya kimaadili yanayoongoza mwenendo wa watu wafanyao kazi ya Jaji au ya Hakimu; "madaraka ya kazi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano" maana yake itabidi ifahamike kwa mujibu wa maana ya kawaida ya maneno hayo na ni pamoja na utumishi katika Majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Muungano na katika Jeshi la Polisi au jeshi linginelo lililoundwa kwa mujibu wa Sheria; "mahakama" maana yake ni mahakama yoyote yenye mamlaka katika Jamhuri ya Muungano isipokuwa mahakama iliyoundwa kwa amri ya jeshi; lakini kwa ajili ya ibara ya 13, ya 14 na ya 15 za Katiba hii, itakuwa ni pamoja na mahakama iliyoundwa kwa amri ya jeshi.
"Mahakama Kuu" maana yake ni Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano au Mahakama Kuu ya Zanzibar; "Mambo ya Muungano" maana yake ni mambo yote ya umma ambayo yametajwa na ibara ya 4 ya Katiba hii kuwa ni Mambo ya Muungano; "Mamlaka ya Nchi" ni pamoja na Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano, pamoja na Serikali na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar; "Mwanasheria Mkuu" maaana yake ni Mwanasheria mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano aliyetajwa katika ibara ya 59; "Serikali" maana yake ni pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au Halmashauri ya Wilaya au ya Mji, na pia mtu yeyote anayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya Serikali au Halmashauri; "Serikali za Mitaa" maana yake ni vyombo vya kiserikali vilvyoundwa kwa mujibu wa ibara ya 145 ya Katiba hii kwa madhumuni ya kutekeleza madaraka ya umma; "Tanzania Bara" maana yake ni eneo lote la Jamhuri ya Muungano ambalo zamani lilikuwa eneo la Jamhuri ya Tanganyika; "Tanzania Zanzibar" maana yake ni eneo lote la Jamhuri ya Muungano ambalo zamani lilikuwa eneo la Jamhuri ya watu wa Zanzibar na ambalo kabla ya Sheria hii kutungwa liliitwa Tanzania Visiwani; "Uchaguzi Mkuu" au "uchaguzi unaofanywa na wananchi" maana yake ni uchaguzi wa Rais na uchaguzi wa Wabunge wanaowakilisha wilaya za uchaguzi unaaofanywa baada ya Bunge kuvunjwa; "Ujamaa" au "Ujamaa na Kujitegemea" maana yake ni misingi ya maisha ya jamii ya kujenga Taifa linalozingatia demokrasia, kujitegemea, uhuru, haki, usawam udugu na umoja wa wananchi wa Jamhuri ya Muungano; "Waziri" maana yake ni Mbunge aliyekabidhiwa madaraka ya kazi ya Waziri, isipokuwa Naibu Waziri, na maana hiyo itatumika pia kwa Makamu wote wa Rais; "Zanzibar" maana yake ni sawa na maana ya Tanzania Zanzibar.
(2)Kanuni zifuatazo zitatumika kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya Katiba, yaani -
(a)kila yanapotajwa madaraka ya Rais, ifahamike kuwa mdaraka yanayohusika ni pamoja na mamlaka ya kutekeleza shughuli za kazi mbalimbali na vile vile wajibu wa kutekeleza shughuli na kazi mbali mali kama Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, na pia mamlaka mengine kama hayo au wajibu mwingine kama huo ikiwa imeelezwa katika Katiba hii au katika sheria nyingine yoyote kwamba mamlaka hayo mengine ni ya Rais au kwamba wajibu huo mwingine ni wa Rais;
(b)kila yanapotajwa madaraka ya kazi katika utumishi wa Serikali, ifahamike kuwa kazi inayohusika ni kazi katika Utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Mungano isipokuwa kama imeelezwa vingine, na kila inapotajwa Idara ya Serikali ifahamike kuwa idara inayohusika ni idara ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, isipokuwa kama imeelezwa vingine;
(c)iwapo kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii kuna jambo lolote linalotakiwa litekelezwe au lishughulikiwe na chama chochote cha siasa, basi, jambo hilo litatekele zwa au litashughulikiwa na chama hicho kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na chama hicho kwa ajili hiyo, na pia kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii au Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo;
(d)kwa madhumuni ya Katiba hii, mtu hatahesabiwa kuwa ana madaraka ya kazi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa sababu tu kwamba anapokea malipo ya uzeeni au malipo mengine ya aina hiyo kwa ajili ya utumishi wake wa zamani katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano au katika Serikali yoyote ya zamani ya Tanzania Bara au katika Jeshi la Ulinzi au la Polisi la Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali ya zamani ya Tanzania Bara au ya Zanzibar;
(e)katika Katiba hii, ila iwapo maelezo yahitaji vingine, kila anapotajwa mtu mwenye dhamana ya kazi fulani kwa kutaja madaraka ya kazi yake, ifahamike kuwa mtu anayehusika ni pamoja na mtu yeyote ambaye ni Kaimu au aliyeteuliwa kwa njia ya halali kushikilia dhamana ya kazi hiyo;
(f)katika Katiba hii, kila yalipotajwa mamlaka ya kumwondoa mtu katika madaraka ya kazi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ifahamike kuwa mamlaka yanayohusika ni pamoja na mamlaka yaliyotolewa kwa mujibu wa masharti ya Sheria yoyote yanayomtaka mtu huyo au yanayomruhusu mtu huyo kustaafu:
Isipokuwa kwamba maelezo ya Kanuni hii yasifahamike kuwa yanampa mtu yeyote mamlaka ya kumtaka Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama Kuu au Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu astaafu;
(g)katika Katiba hii, kila ilipotajwa sheria ambayo inabadilisha au kufuta sheria nyingine, ifahamike kuwa sheria inayohusika ni pamoja na sheria ambayo inarekebisha sheria hiyo nyingine au ambayo inaendeleza kutumika kwa hiyo sheria nyingine, ama bila mabadiliko au baada ya kubadilishwa au kurekebishwa; au sheria ambayo inaweka masharti mapya katika sheria nyingine.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.52 na 53 Sheria ya 1992 Na.4 ib.38 Sheria ya 2000 Na.3 ib.19 Sheria Na.5 ya Mwaka 1992 Sura 512;
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.