Ibara 150
Maelezo kuhusu utaratibu wa kukabidhi madaraka ya kazi katika Utumishi wa Serikali
Mengineyo
(1)Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya Katiba hii kuhusu utaratibu wa kukabidhi madaraka ya kazi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ifahamike kuwa mtu yeyote mwenye mamlaka, kwa mujibu wa Katiba hii, ya kumteua au kumchagua mtu mwingine kushika madaraka ya kazi fulani anao pia uwezo wa kumteua au kumchagua kaimu au mtu ambaye atashikilia kwa muda na kutekeleza madaraka ya kazi hiyo:
Isipokuwa kwamba maelezo hayo hayatatumika kwa madaraka ya kazi ya Waziri, Naibu Waziri, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama Kuu, Mjumbe wa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi au Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi.
(2)Kanuni zifuatazo zitatumika pia kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya Katiba hii kuhusu utaratibu wa kukabidhiana madaraka ya kazi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, yaani:
(a)iwapo kuna mtu mwenye madaraka ya kazi fulani aliyokabidhiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na mtu huyo yupo likizoni na wakati huo huo anangojea kuacha kazi hiyo, basi anaweza kuteuliwa mtu mwingine na kukabidhiwa madaraka ya kazi hiyo, bila ya kujali kuwapo kwa yule mtu anayengojea kuacha kazi hiyo;
(b)iwapo kuna watu wawili au zaidi ambao kwa wakati mmoja wote wanashika madaraka ya kazi fulani kutokana na uteuzi wao uliofanywa kwa mujibu wa Kanuni iliyoelezwa katika aya ya (a) ya ibara hii ndogo, basi katika hali hiyo kukitokea haja ya kutekeleza shughuli yoyote inayohusika na madaraka ya kazi hiyo yule mtu wa mwisho kuteuliwa ndiye atakayehesabiwa kuwa mtu pekee mwenye dhamana ya kazi hiyo;
(c)iwapo mtu ameteuliwa, kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, kuwa kaimu au kushikilia madaraka ya kazi fulani wakati mtu maalum aliyeteuliwa kushika madaraka ya kazi hiyo anashindwa kutekeleza shughuli zinazohusika na kazi hiyo, basi haitaruhusiwa kufanya uchunguzi wowote au kutoa hoja yoyote juu ya uteuzi wa huyo kaimu eti kwa sababu kwamba huyo mtu maalum aliyeteuliwa kushika madaraka ya kazi hiyo anashindwa kutelekeza shughuli zinazohusika na kazi hiyo.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1979 Na.14 ib.12 Sheria ya 1980 Na.1 ib.16 na Sheria ya 1984 Na.15 ib.52
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.