Ibara 113
Madaraka ya kuajiri Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama
Utoaji Haki katika Jamhuri ya Muungano, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Tume ya Kuajiri ya Mahakama ya Tanzania Bara, Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano · Madaraka ya Kuajiri Mahakimu na Watumishi Wengine wa Mahakama za Tanzania Bara na Tume ya Kuajiri ya Mahakama
(1)Bila ya kuathiri masharti ya Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge inayohusika na suala la kuajiri Mahakimu na Watumishi wengineo wa Mahakama mgawanyo wa madaraka kwa ajili ya suala hilo utakuwa ifuatavyo:
(a)madaraka ya kuwaajiri watu wa kushika madaraka ya aina zilizotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara hii (pamoja na madaraka ya kuwathibitisha watu hao kazini na kuwapandisha vyeo) yatakuwa mikononi mwa Rais;
(b)madaraka ya kudhibiti nidhamu ya watu hao na madaraka ya kuwaondoa kazini yatakuwa mikononi mwa Tume ya Kuajiri iliyotajwa katika ibara ya 112 ya Katiba hii.
(2)Madaraka yanayohusika na masharti ya ibara hii ni madaraka ya Msajili wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Naibu wa Msajili huyo wa daraja lolote, madaraka ya Msajili wa Mahakama Kuu na Naibu wa Msajili huyo wa daraja lolote, madaraka ya Hakimu Mkazi na Hakimu wa aina nyingine yoyote, na madaraka ya aina nyingine yoyote yanayohusika na Mahakama yoyote (isipokuwa Mahakama ya Kijeshi) itakayotajwa na Sheria iliyotungwa na Bunge kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1979 Na.14 Ib.7 Sheria ya 1985 Na.15 ib.22 Sheria ya 1985 Na.24 ib….
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.