Wakili Msomi

Ibara 149

Maelezo ya mambo yanayohusika na madaraka ya kazi mbalimbali zilizoanzishwa na Katiba hii

Mengineyo

(1)Mtu yeyote mwenye dhamana ya kazi yoyote iliyoanzishwa na Katiba hii (pamoja na kazi ya Waziri, Naibu Waziri au Mbunge, isipokuwa Mbunge ambaye ni Mbunge kwa mujibu wa madaraka ya kazi yake, aweza kujiuzulu kwa kutoa taarifa iliyoandikwa na kutiliwa sahihi kwa mkono wake, kwa kufuata masharti yafuatayo:

(a)iwapo mtu huyo aliteuliwa au alichaguliwa na mtu mmoja, basi taarifa hiyo ya kujiuzulu atawasilisha kwa mtu huyo aliyemteua au aliyemchagua, au iwapo aliteuliwa au alichaguliwa na kikao cha watu, basi taarifa hiyo ya kujiuzulu ataiwasilisha kwenye kikao hicho;

(b)iwapo mtu huyo ni Rais, basi taarifa hiyo ya kujiuzulu ataiwasilisha kwa Spika;

(c)iwapo mtu huyo ni Spika au Naibu wa Spika wa Bunge, basi taarifa hiyo ya kujiuzulu ataiwasilisha kwenye Bunge; na

(d)iwapo mtu huyo ni Mbunge, basi taarifa hiyo ya kujiuzulu ataiwasilisha kwa Spika.

(2)Mtu aliyetoa taarifa ya kujiuzulu kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (1) ya ibara hii, atahesabiwa kuwa amejiuzulu tangu siku ile ambayo taarifa yake ya kujiuzulu itakapopokelewa na mtu anayehusika au kikao kinachohusika na itakapopokelewa na mtu yeyote aliyeruhusiwa kuipokea taarifa hiyo na mtu anayehusika au kikao kinachohusika, lakini kama taarifa hiyo ya kujiuzulu imeeleza kwamba mtu huyo atajiuzulu tangu siku nyingine baada ya taarifa hiyo kupokelewa na mtu anayehusika au kikao kinachohusika, basi mtu huyo atahesabiwa kuwa amejiuzulu tangu siku hiyo nyingine ya baadaye.

(3)Iwapo mtu yeyote mwenye dhamana ya kazi yoyote iliyoanzishwa na Katiba hii (pamoja na kazi ya Waziri, Naibu Waziri au Mbunge, isipokuwa Mbunge ambaye ni Mbunge kwa mujibu wa madaraka ya kazi yake) amejiuzulu, basi ikiwa anazo sifa zote zinazohitajika na kwa kila hali anastahili, aweza kuteuliwa au kuchaguliwa tena kushika madaraka ya kazi hiyo kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.

(4)Masharti yaliyomo katika ibara ndogo ya (3) ya ibara hii hayatamzuia mtu ambaye ni Rais kuchaguliwa tena kuwa Rais wakati bado ameshika madaraka ya kazi ya Rais.

Marejeo ya marekebisho: Sheria za 1980 Na.1 ib.16; na Sheria ya 1984 Na.15 ib.52 Sheria ya 1992 Na.4 ib.37

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.