Wakili Msomi

Ibara 148

Madaraka ya Amiri Jeshi Mkuu

Majeshi ya Ulinzi

(1)Bila ya kuathiri masharti yatakayowekwa na sheria yoyote iliyotungwa na Bunge, miongoni mwa madaraka ya Rais akiwa kama Amiri Jeshi Mkuu ni kuyaamuru majeshi ya nchi yatende mambo yanayohusika na vita vya ulinzi wa Jamhuri ya Muungano, mambo ya kuokoa maisha na mali ya watu katika hali ya hatari na mambo mengineyo ambayo Amiri Jeshi Mkuu ataona yahitajika, na kwa ajili hiyo Amiri Jeshi Mkuu aweza kuyaamuru hayo majeshi yatende mambo hayo ama ndani au nje ya Tanzania.

(2)Bila ya kuathiri masharti yatakayowekwa na sheria iliyotungwa na Bunge, madaraka juu ya mambo yafuatayo yatakuwa mikononi mwa Amiri Jeshi Mkuu, yaani-

(a)madaraka ya kuwateua viongozi katika majeshi ya ulinzi ya Jamhuri ya Muungano;

(b)madaraka ya kuwateua watu watakaojiunga na majeshi ya ulinzi na madaraka ya kuwaondoa jeshini wanajeshi;

(c)madaraka ya kuwateua wanajeshi watakaoongoza vikosi mbali mbali vya majeshi ya ulinzi; na

(d)madaraka ya kumwamuru mwanajeshi yeyote asitumie madaraka yoyote aliyokabidhiwa na ambayo yanaambatana na kuwa kwake mwanajeshi.

(3)Jambo lolote atakalotenda mwanajeshi yoyote kinyume cha amri iliyotolewa na Amiri Jeshi Mkuu kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (1) na (2) ya ibara hii litakuwa batilifu.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.49

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.