Ibara 36
Mamlaka ya kuanzisha na kuwateua watu wa kushika nafasi za madaraka
Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Rais
(1)Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na ya sheria nyingine yoyote, Rais atakuwa na mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(2)Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali, na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo zimetajwa katika Katiba hii au katika sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa kwa uteuzi unaofanywa na Rais.
(3)Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (2), masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na ya sheria yoyote inayohusika, mamlaka ya kuwateua watu wengine wote wasiokuwa viongozi wala watendaji wakuu, kushika nafasi za madaraka katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, na pia mamalaka ya kuwapandisha vyeo watu hao, kuwaondoa katika madaraka, kuwafukuza kazi na mamlaka ya kudhibiti nidhamu ya watu waliokabidhiwa madaraka, yatakuwa mikononi mwa Tume za Utumishi na mamlaka mengineyo yaliyotajwa na kupewa madaraka kuhusu nafasi za madaraka kwa mujibu wa Katiba hii au kwa mujibu wa sheria yoyote inayohusika.
(4)Masharti ya ibara ndogo ya (2) na ya (3) hayatahesabiwa kuwa yanamzuia Rais kuchukua hatua za kudhibiti nidhamu ya watumishi na utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.9 Sheria ya 2000 Na.3 ib.6
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.