Ibara 84
Spika na Mamlaka yake
Bunge la Jamhuri ya Muungano · Utaratibu, Madaraka na Haki za Bunge
(1)Kutakuwa na Spika wa Bunge ambaye atachaguliwa na Wabunge kutoka miongoni mwa watu ambao ni Wabunge au wenye sifa za kuwa Wabunge; atakuwa ndiye kiongozi wa Bunge na atawakilisha Bunge katika vyombo na vikao vingine vyote nje ya Bunge.
(2)Waziri, Naibu Waziri au mtu mwenye madaraka ya aina nyingine yoyote itakayotajwa na Sheria iliyotungwa na Bunge kwa madhumuni ya ibdara hii, hataweza kuchaguliwa kuwa Spika.
(3)Mtu yeyote atakayechaguliwa kuwa Spika atatakiwa, kabla ya kumaliza siku kumi na tano tangu kuchaguliwa kwake, kuwasilisha kwa Rais tamko rasmi kwamba hajapoteza sifa za uchaguzi kwa mujibu wa masharti ya aya ya (d) ya ibara ndogo ya
(2)ya ibara ya 67. Tamko hilo litatolewa kwa kutumia fomu maalum itakayowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.
(4)Rais atawasilisha kwa Kamishna wa Maadili nakala moja ya kila tamko rasmi lililowasilishwa kwake kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (3) ya ibara hii.
(5)Spika atatakiwa kuwasilisha kwa Rais nakala mbili za taarifa rasmi ya maelezo ya mali ya huyo Spika na, kadri itakavyokuwa, mali ya mke au mume wake. Spika atatoa taarifa hiyo kwa kutumia fomu maalum iliyowekwa kwa ajili hiyo kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge na atatoa taarifa ya namna hiyo mara kwa mara kadri itakavyoagiza sheria hiyo.
(6)Masharti ya ibara ndogo ya (2) na ya (3) ya ibara ya 70 yatatumika pia, kwa kadri itakavyowezekana, kwa taarifa ya mali yoyote itakayotolewa na Spika, kwa mujibu wa masharti ya ibara hii.
(7)Spika atakoma kuwa Spika na ataacha kiti cha Spika litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo -
(a)iwapo mtu huyo alichaguliwa kutoka miongoni mwa Wabunge, basi ikiwa atakoma kuwa Mbunge kwa sababu yoyote ambayo haihusiki na kuvunjwa Bunge; au
(b)ikiwa kutatokea jambo lolote ambalo, kama asingekuwa Spika, lingemfanya mtu huyo asiwe na sifa za uchaguzi au apoteze sifa za uchaguzi wa Spika; au
(c)Bunge litakapokutana kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanywa baada ya Bunge kuvunjwa,
lakini masharti ya aya hii yatatumika bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (4) ya ibara ya 90 ya Katiba hii; au
(d)ikiwa mtu huyo ataondolewa kwenye madaraka ya Spika kwa azimio la Bunge lililoungwa mkono na Wabunge amabo idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote; au
(e)ikiwa mtu huyo atashindwa kuwasilisha kwa Rais tamko rasmi kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo
(5)ya ibara hii; au
(f)ikiwa mtu huyo atapatikana na hatia kwa kosa la kutoa habari za uongo, kwa kiapo kinyume cha sheria ya Kanuni ya jinai, kuhusu tamko rasmi lolote lililotolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (3) ya ibara hii; au
(g)ikiwa mtu huyo atashindwa kuwasilisha kwa Rais taarifa ya mali kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (5) ya ibara hii kabla ya kumalizika muda uliowekwa kwa ajili hiyo kwa mujibu wa sheria iliotungwa na Bunge;
(h)ikiwa itathibitika kuwa mtu huyo amevunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;
(8)Hakuna shughuli yoyote itakayotekelezwa katika Bunge (isipokuwa uchaguzi wa Spika) wakati wowote ambao kiti cha Spika kitakuwa ki wazi.
(9)Mtu yeyote ambaye si Mbunge atakayechaguliwa kuwa Spika, atatakiwa, kabla ya kuanza kutekeleza madaraka yake, kuapishwa katika Bunge kiapo cha uaminifu.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.14 Sheria ya 1992 Na.4 ib.31 Sheria ya 1995 Na.12 ib.15
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.