Ibara 85
Naibu wa Spika
Bunge la Jamhuri ya Muungano · Utaratibu, Madaraka na Haki za Bunge
(1)Kutakuwa na Naibu wa Spika wa Bunge ambaye atachaguliwa na wajumbe kutoka miongoni mwa Wabunge.
(2)Waziri, Naibu Waziri au mtu mwenye madaraka ya aina nyingine yoyote itakayotajwa na Sheria iliyotungwa na Bunge kwa madhumuni ya ibara hii, hataweza kuchaguliwa kuwa Naibu wa Spika.
(3)Wabunge watamchagua Naibu wa Spika nyakati zifuatazo-
(a)Bunge litakapokutana kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu au mapema iwezekanavyo baada ya wakati huo; na
(b)katika kikao cha kwanza cha Bunge baada ya kiti cha Naibu wa Spika, kuwa wazi kwa sababu yoyote isiyohusika na Bunge kuvunjwa au mapema iwezekanavyo baada ya kikao hicho.
(4)Naibu wa Spika, atakoma kuwa Naibu wa Spika na ataacha kiti cha Naibu wa Spika litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo-
(a)ikiwa mtu huyo atakoma kuwa Mbunge; au
(b)ikiwa kutatokea jambo lolote ambalo kama asingekuwa Naibu wa Spika, lingemfanya mtu huyo asiwe na sifa za uchaguzi au apoteze sifa za uchaguzi wa Naibu wa Spika; au
(c)ikiwa mtu huyo ataondolewa kwenye madaraka ya Naibu wa spika kwa azimio la Bunge.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.14
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.