Ibara 13
Usawa mbele ya sheria
Jamhuri ya Muungano, Vyama vya Siasa, Watu na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea · Haki na Wajibu Muhimu
(1)Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
(2)Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.
(3)Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na Mahakama na vyombo vinginevyo vya Mamlaka ya Nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.
(4)Ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa kazi au shughuli yoyote ya Mamlaka ya Nchi.
(5)Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara hii neno "kubagua" maana yake ni kutimiza haja, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia utaifa wao, kabila, pahala walipotokea, maoni yao ya kisiasa, rangi, dini, jinsia au hali yao ya maisha kwa namna ambayo watu wa aina fulani wanafanywa au kuhesabiwa kuwa dhaifu au duni na kuwekewa vikwazo au masharti ya vipingamizi ambapo watu wa aina nyingine wanatendewa tofauti au wanapewa fursa au faida iliyoko nje ya masharti au sifa za lazima, isipokuwa kwamba neno "kubagua" halitafafanuliwa kwa namna ambayo itaizuia Serikali kuchukua hatua za makusudi zenye lengo la kurekebisha matatizo katika jamii.
(6)Kwa madhumuni ya kuhakikisha usawa mbele ya sheria, Mamlaka ya Nchi itaweka taratibu zinazofaa au zinazozingatia misingi kwamba -
(a)wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa mahakama au chombo kinginecho kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na pia haki ya kukata rufaa au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo hicho kingenecho kinachohusika;
(b)ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo;
(c)ni marufuku kwa mtu kuadhibiwa kwa sababu ya kitendo chohote ambacho alipokitenda hakikuwa ni kosa chini ya sheria, na pia kwamba ni marufuku kwa adhabu kutolewa ambayo ni kubwa kuliko adhabu iliyokuwapo wakati kosa linalohusika lilipotendwa;
(d)kwa ajili ya kuhifadhi haki ya usawa wa binadamu, heshima ya mtu itatunzwa katika shughuli zote zinazohusu upelelezi na uendeshaji wa mambo ya jinai na katika shughuli nyinginezo ambazo mtu anakuwa chini ya ulinzi bila uhuru, au katika kuhakikisha utekelezaji wa adhabu;
(e)ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.6 Sheria ya Na.4 ya 1992 ib.8 Sheria ya 2000 Na.3 ib.5
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.