Wakili Msomi

Ibara 30

Mipaka kwa haki, uhuru na hifadhi kwa haki na wajibu

Jamhuri ya Muungano, Vyama vya Siasa, Watu na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea · Haki na Wajibu Muhimu

(1)Haki na uhuru wa binadamu ambavyo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba hii havitatumiwa na mtu mmoja kwa maana ambayo itasababisha kuingiliwa kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma.

(2)Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika Sehemu hii ya Katiba hii, yanayofafanua misingi ya haki, uhuru na wajibu wa binadamu, hayaharamishi sheria yoyote iliyotungwa wala kuzuia sheria yoyote kutungwa au jambo lolote halali kufanywa kwa mujibu wa sheria hiyo, kwa ajili ya -

(a)kuhakikisha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru na haki za watu binafsi;

(b)kuhakikisha ulinzi, usalama wa jamii, amani katika jamii, maadili ya jamii, afya ya jamii, mipango ya maendeleo ya miji na vijiji, ukuzaji na matumizi ya madini au ukuzaji na uendelezaji wa mali au maslahi mengineyo yoyote kwa nia ya kukuza manufaa ya umma;

(c)kuhakikisha utekelezaji wa hukumu au amri ya mahakama iliyotolewa katika shauri lolote la madai au la jinai;

(d)kulinda sifa, haki na uhuru wa watu wengine au maisha binafsi ya watu wanaohusika katika mashauri mahakamani, kuzuia kutoa habari za siri; kutunza heshima, mamlaka na uhuru wa mahakama;

(e)kuweka vizuizi, kusimamia na kudhibiti uanzishaji, uendeshaji na shughuli za vyama na mashirika ya watu binafsi nchini; au

(f)kuwezesha jambo jingine lolote kufanyika ambalo linastawisha au kuhifadhi maslahi ya taifa kwa jumla.

(3)Mtu yeyote anayedai kuwa sharti lolote katika Sehemu hii ya Sura hii au katika sheria yoyote inayohusu haki yake au wajibu kwake, limevunjwa, linavunjwa au inaelekea litavunjwa na mtu yeyote popote katika Jamhuri ya Muungano, anaweza kufungua shauri katika Mahakama Kuu.

(4)Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii, Mahakama Kuu itakuwa na mamlaka ya kusikiliza kwa mara ya kwanza na kuamua shauri lolote lililoletwa mbele yake kwa kufuata ibara hii; na Mamlaka ya Nchi yaweza kuweka sheria kwa ajili ya-

(a)kusimamia utaratibu wa kufungua mashauri kwa mujibu wa ibara hii;

(b)kufafanua uwezo wa Mahakama Kuu katika kusikiliza mashauri yaliyofunguliwa chini ya ibara hii;

(c)kuhakikisha utekelezaji bora wa madaraka ya Mahakama Kuu, hifadhi na kutilia nguvu haki, uhuru na wajibu kwa mujibu wa Katiba hii.

(5)Endapo katika shauri lolote inadaiwa kwamba sheria yoyote iliyotungwa au hatua yoyote iliyochukuliwa na Serikali au mamlaka nyingine inafuta au inakatiza haki, uhuru na wajibu muhimu zitokanazo na ibara ya 12 hadi 29 za Katiba hii, na Mahakama Kuu inaridhika kwamba sheria au hatua inayohusika, kwa kiwango inachopingana na Katiba ni batili au kinyume cha Katiba basi Mahakama Kuu ikiona kuwa yafaa au hali au masilahi ya jamii yahitaji hivyo, badala ya kutamka kuwa sheria au hatua hiyo ni batili, itakuwa na uwezo wa kuamua kutoa fursa kwa ajili ya Serikali au mamlaka nyingine yoyote inayohusika kurekebisha hitilafu iliyopo katika sheria inayotuhumiwa au hatua inayohusika katika muda na kwa jinsi itakavyotajwa na Mahakama Kuu, na sheria hiyo au hatua inayohusika itaendelea kuhesabiwa kuwa ni halali hadi ama marekebisho yatakapofanywa au muda uliowekwa na Mahakama Kuu utakapokwisha, mradi muda mfupi zaidi ndio uzingatiwe.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.6 Sheria ya 1994 Na.34 ib.6

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.