Wakili Msomi

Ibara 99

Utaratibu wa kutunga Sheria kuhusu mambo ya fedha

Bunge la Jamhuri ya Muungano · Utaratibu, Madaraka na Haki za Bunge

(1)Bunge halitashughulikia jambo lolote kati ya mambo yanayohusika na ibara hii isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na Bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye Bunge na Waziri.

(2)Mambo yanayohusika na ibara hii ni haya yafuatayo:-

(a)Muswada wa Sheria kwa ajili ya lolote kati ya mambo yafuatayo:-

(i)kutoza kodi au kubadilisha kodi kwa namna nyingine yoyote isipokuwa kupunguza;

(ii)kuangiza kwamba malipo au matumizi ya fedha yafanywe kutokana na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au mfuko wa Serikali mwingine wowote au kubadilisha kiwango hicho na namna nyingine yoyte isipokuwa kupunguza;

(iii)kuagiza kwamba malipo au matumizi ya fedha yafanywe kutokana na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au mfuko wa Serikali mwingine wowote wakati ikifahamika kwamba fedha iliyomo katika mifuko hiyo haikupangiwa itolewe kwa ajili ya malipo au matumizi hayo, au kuagiza kwamba malipo au matumizi yanayofanywa kutokana na mifuko hiyo yaongezwe;

(iv)kufuta au kusamehe deni lolote linalotakiwa lilipwe kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano;

(b)hoja au mabadiliko yoyote ya Hoja kwa ajili ya lolote kati ya mambo yaliyoelezwa katika aya ya (a) ya ibara hii ndogo.

(3)Masharti ya ibara hii yatatumika kwa muswada wowote uliowasilishwa kwenye Bunge au Hoja yoyote iliyotolewa katika Bunge na Waziri au Naibu Waziri.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.14

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.