Wakili Msomi

Ibara 137

Utaratibu wa kuidhinisha matumizi ya fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali

Masharti Kuhusu Fedha za Jamhuri ya Muungano · Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano

(1)Rais atatoa maagizo kwa watu wanaohusika kwamba watengeneze na kuwasilisha kwenye Bunge katika kila mwaka wa fedha wa Serikali, makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kipindi cha mwaka wa fedha unaofuata.

(2)Baada ya Bunge kuyakubali makadirio ya matumizi (mbali na matumizi ambayo yameidhinishwa ama na Katiba hii au sheria nyingine yoyote kuwa yatokane na fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali) kutawasilishwa kwenye Bunge Muswada ambao utaitwa Muswada wa Sheria ya Matumizi ya fedha za Serikali, kwa ajili ya kuidhinisha matumizi ya fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali, na fedha hizo zitatolewa kulipa gharama za shughuli mbalimbali za Serikali zinazohusika na makadirio hayo.

(3)Ikiwa katika mwaka wa fedha wowote inaonekana kwamba: Fedha za matumizi zilizoidhinishwa na sheria ya matumizi ya Fedha za Serikali kwa ajili ya shughuli fulani hazitoshi au kwamba imekuwa lazima kulipa gharama za shughuli ambayo haikupangiwa fedha za matumizi kwa mujibu wa sheria; au Kuna fedha ambazo zimetumiwa kwa ajili ya shughuli fulani kwa kiasi kinachozidi kiwango cha matumizi yaliyoidhinishwa na sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali kuhusu shughuli hiyo au kwamba fedha zimetumiwa kulipia gharama za shughuli ambayo haikupangiwa fedha za matumizi kwa mujibu wa Sheria, kutawasilishwa kwenye Bunge makadirio ya matumizi ya nyongeza au, kadri itakavyokuwa, maelezo ya matumizi ya ziada, na baada ya Bunge kuyakubali hayo Makadirio ya matumizi ya nyongeza au maelezo ya matumizi ya ziada, kutawasilishwa kwenye Bunge Muswada wa Sheria ya Matumizi ya fedha za Serikali kwa ajili ya kuidhinisha matumizi ya fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali na fedha hizo zitatumiwa kulipia gharama za shughuli zinazohusika na hayo makadirio au maelezo.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.43

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.