Ibara 136
Masharti ya kutoa fedha za matumizi kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali
Masharti Kuhusu Fedha za Jamhuri ya Muungano · Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano
(1)Fedha hazitatolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali kwa ajili ya matumizi ila kwa mujibu wa masharti yafuatayo:-
(a)fedha hizo ziwe kwa ajili ya matumizi ambayo yameidhinishwa yatokane na fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali na idhini hiyo iwe imetolewa na Katiba hii au sheria nyingine yoyote;
(b)fedha hizo ziwe kwa ajili ya matumizi ambayo yameidhinishwa ama na sheria ya Matumizi ya Serikali iliyotungwa mahsusi na Bunge au sheria iliyotungwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 140 ya Katiba hii.
(2)Fedha zilizomo katika mfuko maalum wowote wa serikali, ukiachilia mbali Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali, hazitatolewa kutoka mfuko huo kwa ajili ya matumizi ila mpaka matumizi hayo yawe yameidhinishwa na sheria.
(3)Fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali hazitatolewa kutoka Mfuko huo kwa ajili ya matumizi ila mpaka matumizi hayo yawe yameidhinishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na pia kwa sharti kwamba fedha hizo ziwe zimetolewa kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwa ajili hiyo kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.43
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.