Wakili Msomi

Ibara 143

Mdhibiti wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano

Masharti Kuhusu Fedha za Jamhuri ya Muungano · Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano

(1)Kutakuwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano.

(2)Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atakuwa na jukumu juu ya mambo yafuatayo:

(a)kuhakikisha kwamba fedha zozote zinazokusudiwa kutolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali matumizi yake yameidhinishwa na kwamba zitatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 136 ya Katiba hii, na iwapo atatosheka kwamba masharti hayo yatatekelezwa ipasavyo, basi ataidhinisha fedha hizo zitolewe;

(b)kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo matumizi yake yameidhinishwa yatokane na fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au fedha ambazo matumizi yake yameidhinishwa na sheria iliyotungwa na Bunge, na ambazo zimetumika, zimetumiwa kwa ajili ya shughuli zilizo husika na matumizi ya fedha hizo na kwamba matumizi hayo yamefanywa kwa kufuata idhini iliyotolewa kuhusu matumizi hayo; na

(c)angalau mara moja kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, hesabu zinazosimamiwa na watumishi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na hesabu za Mahakama zote za Jamhuri ya Muungano na hesabu zinazosimamiwa na Katibu wa Bunge.

(3)Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu na kila mtumishi wa Serikali aliyeruhusiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atakuwa na haki ya kuchunguza vitabu, kumbukumbu, hati nyinginezo zote zinazohusika na hesabu za aina yoyote iliyotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara hii.

(4)Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atawasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hii. Baada ya kupokea taarifa hiyo Rais atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa hiyo na itabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho. Iwapo Rais hatachukua hatua za kuwasilisha taarifa hiyo kwa Spika wa Bunge (au Naibu wa Spika ikiwa kiti cha Spika ki wazi wakati huo au ikiwa kwa sababu yoyote Spika hawezi kutekeleza shughuli za kazi yake) ambaye atawasilisha taarifa hiyo kwenye Bunge.

(5)Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atakuwa pia na jukumu la kutekeleza kazi na shughuli nyingine, na atakuwa na madaraka mengine ya namna mbalimbali, kama itakavyoelezwa na sheria kuhusu hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano au hesabu za vyombo vya Umma au hesabu za Mashirika.

(6)Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2), (3) na (4) ya ibara hii, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali,

lakini maelezo hayo ya ibara hii ndogo hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo.

Marejeo ya marekebisho: Sheria za 1979 Na.14 ib.11 Sheria ya 1984 Na.15 ib.43

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.