Ibara 142
Mishahara ya watumishi fulani wa Serikali kudhaminiwa na Mfuko Mkuu Wa Hazina ya Serikali
Masharti Kuhusu Fedha za Jamhuri ya Muungano · Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano
(1)Watumishi wa Serikali wanaohusika na masharti ya ibara hii watalipwa mishahara na posho kama itakavyoelezwa na sheria iliyotungwa na Bunge.
(2)Fedha za malipo ya mishahara na posho za watumishi wa Serikali wanaohusika na masharti ya ibara hii pamoja na fedha za malipo ya uzeeni na kiinua mgongo kwa wale wanaostahili malipo hayo miongoni mwa watumishi hao zitatolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.
(3)Mshahara anaolipwa mtumishi wa Serikali anayehusika na masharti ya ibara hii pamoja na masharti yake ya kazi havitabadilishwa, baada ya mtumishi huyo kuteuliwa, kwa jinsi ambayo itapunguza masilahi ya mtumishi huyo, lakini maelezo haya hayahusiki na posho anayolipwa mtumishi huyo.
(4)Iwapo mtumishi wa Serikali anayehusika na masharti ya ibara hii ana hiari ya kuchagua kima cha mshahara au aina ya masharti ya kazi, basi kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara ndogo ya (3) ya ibara hii, mshahara wa kima hicho atakachochagua na aina hiyo ya masharti ya kazi atakayochagua vitahesabiwa kuwa vina masilahi zaidi kwake kuliko kima cha mshahara kingine chochote angalichoweza kuchagua au aina ya masharti ya kazi nyingine yoyote angaliyoweza kuchagua.
(5)Masharti ya ibara hii yatatumika kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Mwenyekiti na kila Mjumbe wa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano.
Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.43
Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.