Wakili Msomi

Ibara 140

Mfuko wa Matumizi ya dharura

Masharti Kuhusu Fedha za Jamhuri ya Muungano · Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano

(1)Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kuweka masharti kuhusu mambo yafuatayo:

(a)kuanzisha mfuko wa matumizi ya dharura na kumwezesha Rais au Waziri aliyeteuliwa na Rais kwa ajili hiyo kuazima fedha kutoka mfuko huo kulipia gharama za jambo la haraka na la dharura ambalo halikutazamiwa kutokea na ambalo halikupangiwa fedha zozote za matumizi; na

(b)kumwezesha Rais au Waziri aliyeteuliwa na Rais kwa ajili hiyo kutumia fedha zilizotengwa mahsusi kwa ajili ya shughuli fulani kulipia gharama za jambo la haraka na la dharura kama ilivyoelezwa katika aya ya (a) ya ibara hii ndogo.

(2)Iwapo fedha zimeazimwa kutoka Mfuko wa Matumizi ya dharura au fedha zilitengwa mahsusi kwa ajili ya shughuli fulani zimetumiwa kulipia gharama za jambo la haraka na la dharura, basi kutawasilishwa kwenye Bunge makadirio ya matumizi ya nyongeza, na baada ya Bunge kuyakubali makadirio hayo Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali utakaowasilishwa kwenye Bunge kwa ajili ya kuidhinisha Matumizi hayo ya nyongeza utahakikisha kwamba fedha zozote zilizoazimwa kutoka Mfuko wa Matumizi ya dharura zitarudishwa kwenye Mfuko huo kutokana na fedha za matumizi yatakayoidhinishwa na Muswada huo.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.43

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.