Wakili Msomi

Ibara 90

Kuitishwa kwa mikutano ya Bunge na kuvunjwa kwa Bunge

Bunge la Jamhuri ya Muungano · Utaratibu, Madaraka na Haki za Bunge

(1)Baada ya Uchaguzi Mkuu Rais ataitisha Mkutano wa Bunge Jipya ufanyike kabla ya kupita siku saba tangu kutangazwa matokeo ya huo Uchaguzi Mkuu katika majimbo ya uchaguzi yote isipokuwa katika majimbo yale ambako uchaguzi umefutwa na kufanywa upya.

(2)Rais hatakuwa na uwezo wa kulivunja Bunge wakati wowote, isipokuwa tu-

(a)kama Bunge limemaliza muda wa uhai wake kwa mujibu wa ibara ya 65 ya Katiba hii; au wakati wowote katika miezi kumi na miwili ya mwisho ya uhai wa Bunge, isipokuwa tu kama Spika amepokea taarifa rasmi inayopendekeza kuundwa kwa Kamati Maalum ya Uchunguzi kwa madhumuni ya kumuondoa Rais madarakani kwa mujibu wa ibara ya 46A ya Katiba hii;

(b)kama Bunge limekataa kupitisha Bajeti iliyopendekezwa na Serikali;

(c)kama Bunge limekataa kupitisha Muswada wa sheria kwa mujibu wa idara ya 97(4) ya Katiba hii;

(d)kama Bunge limekataa kupitisha hoja ambayo ni ya msingi katika sera za Serikali, na Rais anaona kwamba njia ya kuendelea kutoka hapo si kumteua Waziri Mkuu mwingine bali ni kuitisha Uchaguzi Mkuu;

(e)endapo, kutokana na uwiano wa uwakilishi wa Vyama vya Siasa katika Bunge, Rais anaona kwamba hakuna uhalali kwa Serikali iliyopo kuendelea kuwapo, na wala haiwezekani kuunda Serikali mpya.

(3)Muda wa maisha ya Bunge ukimalizika Bunge litahesabiwa kuwa limevunjwa; isipokuwa kwamba muda huo ukisha wakati wowote ambapo Jamhuri ya Muungano iko katika vita Bunge laweza mara kwa mara kuongeza muda huo uliotajwa katika ibara ya 65 ya Katiba hii kwa muda usiozidi miezi kumi na miwili mara kwa mara lakini maisha ya Bunge hayawezi kuongezwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo kwa muda unaozidi miaka mitano.

(4)Kukitokea hali ya hatari au kama kuna hali ya hatari ambayo Rais anaona inasababisha kuitisha Mkutano wa Bunge na iwapo wakati huo Bunge limevunjwa na matokeo ya kura zilizo nyingi za Uchaguzi Mkuu hayajatangazwa basi Rais aweza kutoa Taarifa Maalum ya kuitisha Mkutano wa Bunge na kuangiza kwamba Spika na watu wote waliokuwa Wabunge mara tu kabla Bunge halijavunjwa wahudhurie Mkutano huo wa Bunge na watu hao pamoja na huyo Spika, watahesabiwa kuwa ndio Wajumbe wa Bunge kwa madhumuni ya Mkutano huo na watahesabiwa hivyo mpaka usiku wa manane wa siku yatakapotangazwa matokeo ya kura zilizo nyingi za Uchaguzi Mkuu.

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.