Wakili Msomi

Ibara 61

Wakuu wa Mikoa

Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Waziri Mkuu, Baraza la Mawaziri na Serikali

(1)Kutakuwa na Mkuu wa Mkoa kwa kila mkoa katika Jamhuri ya Muungano ambaye, bila ya kuathiri ibara ndogo ya (3), atakuwa ni kiongozi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

(2)Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Bara watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.

(3)Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Zanzibar watateuliwa na Rais wa Zanzibar baada ya kushauriana na Rais.

(4)Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (5), kila Mkuu wa Mkoa, atakuwa na wajibu wa kusimamia utekelezaji wa kazi na shughuli zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika mkoa aliokabidhiwa; na kwa ajili hiyo, atatekeleza kazi na shughuli zote zilizotajwa na sheria, au kwa mujibu wa sheria kama hizi au shughuli za Mkuu wa Mkoa na atakuwa na madaraka yote yatakayotajwa na sheria yoyote iliyotungwa na Bunge.

(5)Pamoja na wajibu na madaraka yake yaliyotajwa kwenye masharti yaliyotangulia ya ibara hii, Mkuu wa Mkoa kwa mkoa wowote katika Tanzania Zanzibar atatekeleza kazi za shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar atakazokabidhiwa na Rais wa Zanzibar, na kwa mujibu wa Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar 1984 au sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1984 Na.15 ib.9

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.