Wakili Msomi

Ibara 46B

Wajibu wa viongozi Wakuu wa vyombo vya Mamlaka ya Utendaji kudumisha Muungano

Serikali ya Jamhuri ya Muungano · Rais

(1)Bila ya kuathiri wajibu wa kila raia uliotajwa katika ibara ya 28 ya Katiba hii, viongozi wakuu wa vyombo vyenye mamlaka ya utendaji katika Jamhuri ya Muungano vilivyotajwa katika, ibara ya 4 ya Katiba hii, watawajibika, kila mmoja wao katika kutekeleza madaraka aliyopewa kwa mujibu wa Katiba hii au Katiba ya Zanzibar, 1984, kuhakikisha kuwa analinda kuimarisha na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano.

(2)Kwa madhumuni ya masharti ya ibara ndogo ya (1), kila mmojwawapo wa viongozi wakuu wa vyombo vyenye mamlaka ya utendaji katika Jamhuri ya Muungano kabla ya kushika madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii ataapa kuitetea na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Katiba hii.

(3)Viongozi Wakuu wanaohusika na masharti ya ibara hii:-

(a)Rais wa Jamhuri ya Muungano;

(b)Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano;

(c)Rais wa Zanzibar, na

(d)Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano.

Marejeo ya marekebisho: Sheria ya 1995 Na.12 ib.5

Source: official text. If anything here differs from the official publication, the official publication prevails.